Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Safari ya Tanzania Kufikia Uchumi wa Kati si Ndoto Tena
Jun 20, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na. Immaculate Makilika

Ni miaka michache imebaki kufikia mwaka 2025, mwaka ambao Tanzania inatarajiwa  kuwa  nchi ya uchumi wa kati.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika hivi karibuni kupitia jarida la Forbes Afrika, Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli anatanabaisha kuwa dira ya maendeleo ni kuwa na Taifa lenye amani na utulivu, kukomesha vitendo vya rushwa, kuwekeza kwenye elimu pamoja na  kujenga  uchumi imara na wenye ushindani.

Rais Magufuli anasema “Kama nchi, dira yetu iko bayana, utawala wangu umedhamiria kuhakikisha Tanzania inafikia ndoto yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kama dira ya maendeleo inavyosema. Nasisitiza watendaji wa Serikali yangu na kwa wananchi kuwa dira yetu itafikiwa kwa ushirikiao wa karibu kati ya sekta binafsi na umma. Kama mlivyoona, nimekuwa jasiri kufanya mabadiliko makubwa ili kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji na kuhakikisha sekta binafsi inakuza uchumi wa nchi hapo baadae”.

Katika ripoti ya Mtazamo wa Kiuchumi Afrika 2018, iliyoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inaonesha kuwa uchumi wa nchi za Afrika umeendelea kuwa imara; ukuaji halisi unaongezeka, ikiashiria uwepo wa Sera madhubuti za uchumi jumla, maendeleo mazuri katika maboresho ya miundo (hususan katika uboreshaji wa miundombinu) na mifumo ya sera nzuri na madhubuti kwa ujumla.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa, mataifa ya Afrika yanatakiwa kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wao na unaotokana na vyanzo mbalimbali ili kuinua Pato la Taifa lifikie viwango linganifu vipya vya ukuaji unaotokana na ubunifu na wenye tija badala ya kutegemea rasilimali asili.

Mikakati ya Sera za uchumi jumla haina budi kulenga katika kuongeza ushindani wa sekta ya nje ili kuepuka athari zitokanazo na kupungua kwa thamani halisi ya sarafu na kunufaika kibiashara, kuimarisha mapato ya ndani, na kuhuisha matumizi ya umma. Ili kufikia malengo haya, mfumo wa uchumi jumla ni lazima uzingatie kwa pamoja mabadiliko ya thamani halisi ya sarafu, ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia mahitaji kikamilifu.

Serikali  inayoongozwa na Rais Magufuli ni mfano halisi wa jitihada na mikakati inayofanywa na nchi za Afrika katika kufikia mapinduzi ya kiuchumi, yanayotajwa katika ripoti ya hiyo ya Mtazamo wa Kiuchumi Afrika mwaka 2018.

Miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini Tanzania kama vile ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa ‘standard gauge’ unaogharimu dola za kimarekani bilioni 14.2 yenye kilometa 2,561 itakayounganisha Bandari ya  Dar es salaam  na nchi  jirani, kuwa ni mradi ambao utakuza fursa za biashara.

Aidha, Katika mahojiano na Jarida la Forbes, Mkurugenzi wa Kampuni ya ASAS, Faraj Abri anasema: “Miradi kama hii ya SGR itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi kutokana na kupungua kwa gharama za uzalishaji na uendeshaji, kupunguza bei ya bidhaa na kuongeza idadi ya bidhaa zitakazosafirishwa kati ya Tanzania na nchi jirani, hali itakayongeza ushirikiano baina ya nchi na nchi na kuimarisha uchumi wa ukanda huu”

Katika kufikia mapinduzi hayo ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, Bandari ya Dar es salaam, imeendelea na mpango wake wa kuongeza ufanisi katika bandari hiyo yaani Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP), kwa kufadhili uwekezaji muhimu,  mpango ambao unalenga kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa bandari hiyo kwa faida ya wadau ambao ni Serikali na watu binafsi.

Kwa upande wa uendelezaji nishati ambayo ni nyenzo muhimu katika uchumi wa viwanda, Waziri wa Nishanti, Dkt. Medard Kalemani anasema “Serikali kupitia sekta ya nishati imedhamiria kufikia uzalishaji wa megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 and megawati 10,000 kufikia mwaka 2025. Ujenzi wa bwawa kwa ajili ya kufua umeme kutoka bonde la Mto Rufiji umeanza ambao utazalisha megawati 2,115 na hatimaye tutafikia malengo yetu”.

Wakati  tukishuhudia kupungua kwa kasi kwa misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo na shauku kubwa ya kupata mikopo ya kugharamia miradi ya miundombinu na sekta za huduma za kijamii, nchi nyingi za Afrika zimeelekeza jitihada katika kupata mikopo kutoka katika masoko ya mitaji ya kimataifa kuweza kupata mahitaji hayo ya fedha, katika kukabiliana na hali hiyo Rais Magufuli ameendelea kuonesha umuhimu wa kukusanya kodi na kujijengea uwezo kutokana na kodi hizo ili kufikia nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Kupitia miradi hii na mingine katika sekta mbalimbali nchini kama vile ya elimu ambayo inatoa fursa ya elimu bure kuanzia shule za msingi hadi kidato cha nne, pamoja na  miradi mingine ya jamii kama maji na huduma za afya imeendelea kuonesha kuwa safari ya Tanzania ya uchumi wa kati si ndoto tena, kwani wananchi wameendelea kupata huduma bora za afya kwa kutumia vipimo vya kisasa vya MRI na CT scan  kuanzia ngazi za vijiji na halmashauri.

Pamoja na ukuaji huo wa uchumi unaokuwa kwa kasi katika nchi nyingi za Afrika, Ripoti ya Mtazamo wa Kiuchumi Afrika 2018, inatabanaisha kuwa, misingi na ustahimilivu wa uchumi imeimarishwa katika nchi kadhaa za Afrika. Miongoni mwa hizo, mapato ya ndani kwa sasa yanazidi yale yanayokusanywa na baadhi ya nchi wenzao wa bara la Asia na Amerika ya Kusini. Hata hivyo, mapato hayo hayatoshelezi mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu na rasilimali watu.

Taifa lenye uchumi imara linategemea ukuaji wa sekta ya viwanda na mawasiliano, katika kufanikisha hilo Serikali kupitia Mamlaka Mawasiliano nchini (TCRA)  imeendelea kuhakikisha huduma za mawasiliano na intaneti zinaenea sehemu kubwa ya nchi.

Mkurugenzi wa TCRA, Injinia James Kilaba anasema: “Asilimia 94 ya wananchi wanapata huduma za simu, lengo hili  limefikiwa kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali za simu nchini”.

Safari ya hii ya Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, si ndoto tena kama ambavyo Rais Magufuli na watendaji wake wa Serikali wamefafanua mapinduzi mbalimbali ya kisekta yaliyofanyika tangu aingie madarakani mwaka 2015.

Tafsiri sahihi ya uwepo wa miradi hii na mingine mingi inayolenga kukuza uchumi kwa kuzalisha viwanda na kutoa fursa za ajira kwa wananchi, miradi ya umeme inayolenga kuzalisha umeme kwa ajili ya matumizi ya ziada na viwandani  itaoongeza uzalishaji, kukuza soko la bidhaa ndani na nje ya nchi na hatimaye kuongeza pato la Taifa, sambaba na kuongeza fursa za uwekezaji kwa wazawa na wageni.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi