Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), imepokea wasilisho la kwanza la mfumo wa kuandaa gharama za kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara uliotengenezwa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ujenzi, Mhandisi Alois Matei ambae ni Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, amesema kuwa kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika kukadiria gharama za kazi za barabara hapa nchini, ambapo changamoto hizo zimekuwa zikiathiri uandaaji wa mipango na bajeti kwa upande wa Wakala za Barabara kwani mara nyingi bajeti za kazi za barabara hutofautiana sana na gharama halisi.
Uhitaji na umuhimu wa kuwa na mfumo kama huu umekuwepo kwa muda mrefu kwa lengo la kutatua changamoto za Wakala wa Barabara, Wakandarasi na hata wataalamu washauri katika kukadiria gharama za miradi ya barabara.
Ni kwa msingi huu Wizara iliielekeza Bodi ya Mfuko wa Barabara kuratibu na kugharamia uundaji wa mfumo huu
hivyo napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Bodi kwa kufanikisha uundwaji wa mfumo huu kwa mafanikio makubwa na kwa wakati.
Vilevile, naupongeza uongozi wa Baraza la Taifa la Ujenzi pamoja na wataalam wake, kwa kazi nzuri iliyotuwezesha kuwa na mfumo huu, amesema Mhandisi Matei.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Mhandisi Rashid Kalimbaga amesema kuwa Baraza la Taifa la Ujenzi, lilipewa kazi ya kutengeneza mfumo huo tangu mwaka 2020 na sasa wanawasilisha kwa mara ya kwanza pendekezo la mfumo huo kabla ya kuanza kutumika.
Mfumo huu utakapokamilika utasaidia kwenye michakato ya manunuzi ya kazi za barabara.
Hii ni kwa sababu Wakala wa Barabara watakuwa na makadirio mazuri ya gharama za miradi husika na hivyo itakuwa rahisi kubaini mkandarasi anayetoa ofa ya chini zaidi ambayo haiakisi gharama halisi kwa kazi husika, amesema Mhandisi Kalimbaga.
Akijibu maswali ya wadau wa mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi, Dkt. Samson Mturi amewatoa wasiwasi wadau hao kuhusu gharama za awali zilizomo kwenye mfumo huo, kwa kuwa zoezi zima la uandaaji limehusisha wataalamu wa barabara, wakadiriaji majenzi, wakandarasi pamoja na wazabuni wa vifaa vya ujenzi.
Nao washiriki wa kikao hicho kwa nyakati mbalimbali, wamepata fursa ya kuuliza maswali kuhusu mfumo huo pamoja na kutoa michango mbalimbali yenye lengo la kuboresha zaidi mfumo huo mpya wa uandaaji gharama za matengenezo pamoja na ujenzi wa barabara mpya.
Kikao cha kwanza cha wasilisho la mfumo wa kuandaa gharama za kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara kimefanyika kwa siku moja jijini Dodoma huku kikihusisha wadau wa mfumo huo kutoka taasisi mbali mbali zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi).