Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Tabora Anzeni Mapema Kuwaanda Wakulima wa Pamba Ili Tupate Mavuno Mazuri.
Sep 10, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Tiganya Vincent, RS-Tabora

Serikali mkoani Tabora imeawaagiza Maafisa Ugani kuanza mapema maandalizi ya kilimo cha pamba kwa wakulima kutoka wilaya tano mkoani hapo zilichaguliwa kulima zao ili waweze kuzalisha pamba nyingi na nzuri kwa ajili viwanda mbalimbali hapa nchini.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri jana wilayani Igunga wakati alipokwenda kujionea hali halisi ya Kiwanda cha Pamba cha Manonga wilayani Igunga ambacho kimekuwa hakifanyi kazi kwa miaka zaidi ya 20 kwa sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa pamba ya kutosha.

Alisema kuwa watendaji wote wanaohusika na usimamizi wa zao la pamba ni vema wakahakikisha kuwa wakulima wanapanda mbegu zinazotakiwa na kwa nafasi inayoshauri kitaalamu na kutimia mbolea na dawa za kuua wadudu zinazotakiwa.

Mwanri alisema kuwa Tabora imepata mbegu bora tani 500 ambazo zitasaidia kusambazwa katika Wilaya ambazo zimechaguliwa kulima zao la Pamba za Kaliua, Urambo, Nzega, Igunga na Uyui.

Alisisitiza pamba itakayolimwa na kuvuna itauzwa kupitia Vyama vya Ushirika na sio vinginevyo ili kuepuka mkulima kunyonywa.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alipiga marufuku matumizi ya mbegu ambazo hazikuidhinishwa na Bodi ya Pamba na kuingiza mkoani hapa dawa ambazo zimepitwa na wakati.

Alisema kuwa atakayebainika atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya sheria ili apate adhabu inayostahili.

Naye Meneja wa Kanda wa Bodi ya Pamba Jones Bwahama alisema kuwa wilaya ya Igunga mkoani Tabora imechaguliwa kuwa kitalu cha taifa cha uzalishaji wa mbegu za zao hilo , hivyo ni vema wataalamu wakawasaidia wakulima kuzingatia maelekezo ya kitaalamu wakati wote wa ulimaji na uvunaji ili kuwezasha maeneo megine yaje kuchukua mbegu.

Alisema kuwa uzembe wowote utakaofanyika na kusababisha uharibifu wa mbegu hiyo utakuwa umekwamisha juhudi za Serikali za kufufua zao la pamba hapa nchini.

Bwahama alitoa wito kwa Kampuni za ununuzi wa pamba katika Wilaya ya Igunga katika kupata mbegu bora, dawa bora kwa ajili ya kuwakopesha wakulima ili waweze kuzalisha pamba nzuri na bora.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo alisema kuwa msimu ujao wanatarajia kuzalisha pamba nyingi zaidi ya mwaka uliopita kwa sababu ulikuwa mwanzo hivi wameongeza nguvu katika kuwatembelea wakulima na kuwahamasisha juu ya kilimo bora cha zao hilo.

Alisema kuwa wanataka kuongeza kutoka kilo 10,700,000 ili ziwe zaidi ya hapo kwa ajili ya kuongeza kipato cha wakazi wa Igunga na Halmashauri yao.

Mwaipopo alisema kuwa ili kufanikisha zoezi hilo viongozi wilayani humo wamejipanga kupita kwa wakulima ili kuwaelimisha ikiwa ni pamoja na kuwaeleza juu ya matumizi ya mbegu bora na dawa za kuua wadudu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.

Naye Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya  Igunga George Kihimbi alisema kuwa wanatarajia kuanza mikutano ya kuelimisha wakulima ili waweze kufuata masharti ulimaji wa zao hilo kwa ajili ya kuwasidia kupata mazao mengi na yenye tija.

Alisema kuwa tayari wameshatayarisha vifaa mbalimbali kufundishia ikiwemo kamba kwa ajili ya upimaji mashamba ambapo watawaelimisha wakulima juu ya ulipandaji wa miche 22,000 katika heka moja ili wapate kilo 600.

Hivi karibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Kassim Majaliwa alikutana  Wakuu wa Mikoa inayolima pamba nchini na kuwaagiza kuhakikisha wanasimamia zao hilo ili lirudi katika hali yake ya siku za nyuma ambalo liliitwa dhahabu nyeupe.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi