Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RC Tabora Amaliza Mgogoro wa Kampuni ya Ujenzi na Wafanyakazi Wake.
Sep 20, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent – RS, TABORA

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amefanikiwa kumaliza mgogoro kati ya waliokuwa wafanyakazi 11 wa Kampuni ya Ujenzi ya Ceytun iliyokuwa ikipanua Uwanja wa Ndege wa Tabora na wamiliki wake juu ya kulipwa madai ya malipo ya muda wa ziada na mapunjo ya mishahara.

Mgogoro huo ulimalizika jana mjini Tabora baada ya Wamiliki wa Kampuni hiyo kukubali na kulipa madeni ya wafanyakazi wake ambapo  malipo yalifanyika mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Mkuu wa Wilaya ya Tabora.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuamuru kuwang’anywa Hati za kusafiria za viongozi wake wawili wa Kampuni hiyo na kuzuiwa kwa vifaa vyake vya  ujenzi baada ya kuonekana kuwa anataka kuondoka bila kulipa malipo ya wafanyakazi hao.

Akizungumza mara baada ya Kampuni hiyo kuwalipa waliokuwa  wafanyakazi wake Mwanri alisema kuwa amelizika na kazi iliyofanyika na hivi sasa wanaweza kuchukua hati zao za kusafiria na wako huru kuondoa vifaa vyao vya ujenzi kwa sababu wamemalizana na watumishi hao bila kinyongo.

Aliomba Kampuni hiyo ikipata kazi nyingine isisite kuwapa ajira waliokuwa wafanyakazi wake licha ya mvutano uliotokea na kuongeza kuwa kilichotekea ndio mwanzo wa kuboresha mahusiano katika siku za baadaye.

Mwanri alisema kuwa uungwana waliouonyesha kukubali kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao na waliokuwa wafanyakazi wao umeonyesha ni Kampuni inayostahili kuendelea kupewa kazi nyingine hapa nchini.

Aliwataka kutofunga milango kwani inawezekana wapo waliokuwa wafanyakazi wao ambao walisahaulika na wameshaondoka na pindi watakapokuja na vielelezo vinavyoonyesha kuwa bado wanadai basi wasaidiwe na walipwe haki zao.

Kwa upande Meneja Mradi wa Kampuni ya Ujenzi ya Ceytun  Ercan Kavaic alisema kuwa hana kinyongo na mfanyakazi yoyote yule na yuko tayari kufanya kazi na mtu yoyote akipata kazi nyingine.

Alisema kuwa Kampuni yake ilikuwa ikihakikisha kila mtumishi anapofikia ukomo wa mkataba wake inamwongeza mshahara wa mwezi mmoja zaidi ya ule uliopo katika mkataba na kumpa cheti cha kutambua mchango wake katika kushirikiana na Kampuni yake.

Kavaic alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa kufanikisha kumalizika kwa tofauti baina ya Kampuni yake na waliokuwa wafanyakazi wake na kuweza kufika muafaka wa kulipa fedha nusu ya zile ambazo walikuwa wamesama za shilingi milioni 20 baada ya uchambuzi walikuta madai ni milioni 10.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake ambaye ni fundi umeme John Mathew alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Mkuu wa Wilaya ya Tabora kwa kusimamia hadi haki yao imepatikana na kuonyesha moyo wao wa uzalendo wa kushughulikia matatizo ya wananchi hata ikibidi kwa nguvu kubwa.

Pia alimshukuru Meneja Mradi wa Kampuni ya Ujenzi ya Ceytun Bw. Kavaic kwa kubali kukaa meza moja ambayo ndio iliyoleta makubaliano na wao kuweza kupata haki yao na wao walisema wako tayari kufanyakazi naye endapo atapewa jukumu jingine la upanuzi wa uwanja wa ndege kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi