Na Ndimmyake Mwakapiso
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mwanza ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. John Mongela, imefanya ziara rasmi katika ukumbi wa BOT kukagua maandalizi ya kikao kazi cha Maofisa Mawasilino Serikali kinachotarajiwa kufungulia na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasimu Majaliwa, Jijini humo.
Akitoa tathmini yake mara baada ya ukaguzi wa ukumbi wa mkutano huo, Mkuu wa Mkoa ameridhishwa na mandalizi yanayoratibiwa kwa pamoja na Idara ya Habari MAELEZO kwa kushirikiana na Uongozi wa Chama cha Maofisa Mawasiliano Serikalini TAGCO.
“Mnakwenda vizuri, naona kila kitu kipo vizuri na kwa maandalizi haya ni imani yangu kuwa mkutano huu utaenda vizuri na msisite kutufahamisha endapo kutakuwa na mabadiliko yoyote”. Alisisitiza Mhe. Mongela
Mapokezi ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, yaliongozwa na Mkurugenzi wa idara ya Habari Maelezo ambaye pia ndiye msemaji mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abasi na viongozi wa chama cha Maofisa Mawasiliano Serikalini TAGCO.
Kikao hicho ni cha siku tano kinachotarajiwa kuanza siku ya Jumatatu, Machi 18 hadi Ijumaa 22, mwaka huu kinachotarajiwa kuwakutanisha zaidi ya Maofisa Mawasiliano 300 kutoka Wizara, Mashirika ya Umma, Taasisi za Serikali, Tawala za mikoa na Serikali za mitaa.