Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu ambapo katika mabadiliko hayo, ameanzisha nafasi ya Naibu Waziri Mkuu na kuifuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Taarifa hiyo imetolewa leo Agosti 30, 2023 na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka huku ikifafanua kuwa baada ya kufutwa kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, zimeundwa wizara mpya mbili ambazo ni Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi. Aidha, Rais Samia ameimarisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuongeza nafasi ya Naibu Waziri na Katibu Mkuu watakaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
“Katika mabadiliko hayo, Mhe. Rais amemteua Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambapo katika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu atakuwa anashughulikia Uratibu wa Shughuli za Serikali”, ilieleza taarifa hiyo.
Mabadiliko mengine madogo ya Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu yamehusu Mawaziri wanne (4), Naibu Mawaziri watano (5), Makatibu Wakuu watatu (3) na Naibu Makatibu Wakuu watatu (3). Vilevile, amewabadilisha wizara baadhi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu.
Katika Uteuzi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Mhe. Jerry William Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Anthony Peter Mavunde, Naibu Waziri wa Kilimo ameteuliwa kuwa Waziri wa Madini, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Innocent Lugha Bashungwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ameteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Mhe. Godfrey Msongwe Kasekenya aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi,
Mhe. Alexander Pastory Mnyeti, Mbunge wa Jimbo la Misungwi ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum (Ruvuma) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Mhe. Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Jimbo la Mkinga ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utali.
Vilevile, uhamisho wa Mawaziri na Naibu Mawaziri umemhusu Mhe. January Yusuf Makamba amehamishwa kutoka Wizara ya Nishati kwenda kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stergomena Lawrence Tax amehamishwa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenda kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa amehamishwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki amehamishwa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI kwenda kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro amehamishwa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana amehamishwa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mhe. Stephen Lujwahuka Byabato amehamishwa kutoka Wizara ya Nishati kwenda kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atakayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
Katika Uteuzi wa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Rais Samia amemteua Prof. Godius Walter Kahyarara aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Geita kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Mhandisi Cyprian John Luhemeja aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Balozi Prof. Kennedy Gastorn kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atakayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
Dkt. Ally Possi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi naUchukuzi (Uchukuzi) kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi, Bw. Ludovick Nduhiye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Mhandisi Mwajuma Juma Waziri ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji.
Uhamisho wa Makatibu Wakuu umemuhusisha Prof. Jamal Adam Katundu ambaye amehamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) kwenda kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe amehamishwa kutoka Wizara ya Afya kwenda kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Dkt. John Anthony Jingu amehamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwenda kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Afya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huu unaanza leo, tarehe 30 Agosti, 2023 ambapo viongozi walioteuliwa wataapishwa tarehe 1 Septemba, 2023 Ikulu Ndogo, Zanzibar, Saa 5:00 Asubuhi.