Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli kuzindua Barabara ya kwanza ya lami Simanjiro. 
Sep 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Prisca Libaga - Arusha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kesho ataizindua rasmi barabara ya kutoka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, KIA hadi vilima vya Mirerani katika eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite Wilayani Simanjiro.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, Mh.rais atawasili uwanja wa ndege wa Kilimanjaro mapema asubuhi na kwenda moja kwa moja Mirerani kwa ajili ya kuzindua  mradi huo.

Barabara ya KIA-Mirerani yenye urefu wa kilometa 26 ndio itakuwa barabara ya kwanza kabisa ya lami kujengwa katika Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara huku serikali ikiahidi kuiunganisha na Makao Makuu ya Wilaya yaliyopo Orkesumet.

Ujenzi wa Barabara hiyo umegharimu jumla ya Tsh.32.2 billioni/- na ulikuwa ukitekelezwa na kampuni ya M/S China Henan International Cooperation Group Company kutoka China, chini ya usimamizi wa kampuni ya LEA International Engineering Company Limited kutoka Canada ikishirikiana na kampuni ya kizalendo ya DOCH Tanzania Limited.

Rais Magufuli ndiye aliyesimika jiwe la msingi wakati mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ulipoanza mwezi Agosti Mwaka 2015 wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa siku ya alhamisi anatarajiwa kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji utakaohudumia wakazi wa maeneo kame ya wilayani Longido mkoani Arusha.

Waziri Mkuu pia atatumia muda huo kuzungumza na wakazi wa miji midogo ya Longido na Namanga mara baada ya kuweka jiwe hilo la msingi.

Aidha siku ya ya Jumamosi, rais Magufuli atawatunuku kamisheni maafisa wa jeshi wanaohitimu katika Chuo cha mafunzo ya kijeshi (TMA) .Hata hivyo, kwa mara ya kwanza kabisa, katika historia, Rais Magufuli atatoa kamisheni hiyo katika uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, tofauti na ilivyozoeleka kwa kamisheni hizo kutolewa chuoni Monduli.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi