[caption id="attachment_41838" align="aligncenter" width="1000"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa mradi wa Ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme KV 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na vituo vya kupooza umeme KV 220/33 katika sherehe zilizofanyika Songea mkoani Ruvuma[/caption]
Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali itaendelea kutekeleza kwa kasi kubwa ujenzi wa miradi ya nishati nchini ikiwemo Mradi wa kufua umeme wa maji katika Mto Rufiji (Stiegler’s Gorges) hatua inayolenga kuwawezesha wananchi wengi kununua umeme kwa gharama nafuu na hivyo kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Akizungumza leo Jumamosi (April 6, 2019) Mkoani Ruvuma wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme ya kilovolti 220 Makambako- Songea, Rais Magufuli alisema Tanzania ina vyanzo vya kutosha vya kuzalisha umeme hivyo malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa inashusha bei ya kununua umeme kwa Watanzania.
Aliongeza kuwa kwa sasa bei ya umeme kwa uniti moja hapa nchini ni Dola za Marekani senti 11 hadi 12, hali ambayo inawaumiza wananchi wa kipato cha chini kwani hali hiyo ni tofauti katika mataifa yanayoendelea ambayo yenyewe hayana vyanzo vingi vya umeme ukilinganisha na Tanzania ambayo ina vyanzo vingi vya uhakika vya uzalishaji wa nishati ya umeme.
[caption id="attachment_41842" align="aligncenter" width="1000"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg wakiminya kitufe kwa pamoja kuashiria uzinduzi wa mradi wa Ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme KV 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na vituo vya kupooza umeme KV 220/33 katika sherehe zilizofanyika Songea mkoani Ruvuma.[/caption] [caption id="attachment_41841" align="aligncenter" width="1000"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg wakiangalia mradi huo wa umeme utakavyosambaza umeme katika maeneo mbalimbali kutoka kutoka Makambako hadi Songea[/caption]Aidha Rais Magufuli alisema kutokana na malengo iliyojiwekea Serikali katika kufikia nchi ya kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha kuwa inakamilisha ujenzi wa miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme ili kuhakikisha kuwa kunawepo na malighafi za kutosha katika viwanda vya ndani na hivyo kulinda masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Nchi yoyote inayotaka kujikwamua kiuchumi ni lazima iwe na uwezo wa kuzalisha nishati ya kutosha ya umeme, hatua hiyo itawezesha kulinda masoko yake ya ndani na kuepuka kununua malighafi kutoka nje ya nchi ambazo huuzwa kwa bei kubwa, hivyo Serikali tumejipanga kufanikisha adhma hii” alisema Rais Magufuli.
[caption id="attachment_41837" align="aligncenter" width="1000"] Moja ya kituo cha kupooza umeme cha Songea.[/caption]Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kupata ushirikiano kutoka katika wadau mbalimbali wa maendeleo katika kufanikisha ujenzi wa miradi mikubwa ya sekta ya nishati ya umeme, ikiwemo mradi wa kufua umeme wa maji katika Mto Rufiji (Stiegler’s Gorges), ambao unatarajia kuzalisha Megawati 2100 na hivyo kuongeza nguvu katika Megawati 1560 zilizopo kwa sasa katika gridi ya Taifa.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa katika miaka michache ijayo, Tanzania inakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 5000 katika gridi ya taifa hatua inayolenga kuvifanya viwanda vingi vilivyopo nchini viweze kuzalisha malighafi kwa ajili ya matumizi ya ndani pamoja na kusafirisha nje ya nchi.
Akizungumzia kuhusu mradi wa umeme wa ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme ya kilovolti 220 Makambako- Songea, Rais Magufuli alisema kupitia mradi huo Serikali imeweza kuokoa kiasi cha Tsh Bilioni 9.8 zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya kuzalisha umeme wa mafuta mazito na kuwataka watendaji wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kusimamia kwa ukamilifu mradi huo ili uweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alisema mradi wa umeme ya kilovolti 220 Makambako- Songea unatarajia kuvinufaisha jumla ya vijiji 122 vyenye jumla ya wakazi 22,000 waliopo katika Wilaya saba za Mikoa ya Njombe na Ruvuma, ambapo kipaumbele kimetolewa katika maeneo yaliyopo jirani na mradi huo.
Alisema hatua za awali za ujenzi wa mradi huo ikiwemo usanifu ulianza mwaka 2000-2008, lakini nguvu kubwa ya utekelezaji wa mradi huo zilianza Desemba 2015 ambapo jumla ya transfoma 300 zimewekwa katika maeneo mbalimbali yaliyopitiwa na mradi huo.
“Ulipoingia madarakani mwaka 2015, Mhe Rais umeweza kupunguza gharama kubwa katika matumizi ya umeme wa kutumia mafuta mazito ikiwemo mradi wa Aggreko, APTL na Symbion ambapo takribani Tsh Bilioni 712 zilikuwa zikitumika kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta hayo” alisema Dkt. Kalemani.
Kwa upande wake, Balozi wa Usiswi nchini Anders Sjoberg alisema Serikali ya Uswisi itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika kutekeleza miradi yote ya maendeleo ambayo imekuwa ikigusa maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
Alisema Serikali ya Uswisi tangu miaka ya 1970 imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na Wakala wa Umeme Vjijini (REA) ambapo wamekuwa wakipeleka umeme kwa wananchi wa maeneo ya vijijini ili kuweza kuwaletea maendeleo yao.