Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Azindua Kanisa na Afanya Harambee ya Kuchangia Ujenzi wa Msikiti Chamwino
Aug 24, 2020
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amezindua Kanisa, nyumba ya Mapadre na Groto katika Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Ikulu Chamwino iliyopo Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

Katika uzinduzi huo, Mhe. Rais Magufuli ameambatana na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya ambaye amelibariki Kanisa, Groto na nyumba ya Mapadre na baadaye kuongoza Misa Takatifu ya Dominika ya 21 ya Mwaka “A” ndani ya Kanisa hilo.

Ujenzi wa Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Ikulu Chamwino, Groto na ukarabati wa nyumba ya Mapadre wa Kanisa hilo ulianza tarehe 08 Juni, 2020 siku moja baada ya Mhe. Rais Magufuli kuhudhuria Ibada ya Fumbo la Utatu Mtakatifu na kisha kuendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa hilo ambapo pamoja nae, Waumini wa Kanisa hilo na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo na Kiislamu wamejitokeza kuchangia na kufanikiwa kukamilisha ujenzi huo.

Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Padre Dkt. Charles Kitima amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa upendo na uamuzi wake wa kufanya ujenzi mkubwa wa Kanisa, Groto na kukarabati nyumba ya Mapadre wa Parokia hiyo ambayo kwa kuwa kwake Ikulu Chamwino ina historia ya kuwahudumia Marais wa Tanzania.

Baba Askofu Mkuu Kinyaiya amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuongoza kazi kubwa iliyofanyika kuiboresha Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Ikulu Chamwino na amemuelezea kuwa ni kiongozi mwenye uthubutu na anayejali watu anaowaongoza.

Katika Ibada hiyo, Baba Askofu Mkuu Kinyaiya amembariki na kumuombea Mhe. Rais Magufuli ili aendelee kuliongoza Taifa vizuri na hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu, na pia amewataka Watanzania wote kushiriki uchaguzi mkuu huku wakidumisha amani na mshikamano, na kuhakikisha wanachagua viongozi wacha Mungu, wanaotafuta uongozi kwa njia za amani, wanaojiamini na wasiotoa rushwa.

Katika salamu zake, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Baba Askofu Mkuu Kinyaiya kwa kuongoza Misa Takatifu na kulibariki Kanisa, Groto na Nyumba ya Mapadre, na pia amewashukuru wote waliojitokeza kuchangia ujenzi na ukarabati huo ambao umefanyika kwa mafanikio makubwa.

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na umoja wa Watanzania ulioneshwa katika ujenzi huo ambapo waliojenga na waliochangia fedha wametoka katika Madhehebu mbalimbali ya Dini.

Akiwa anatoa salamu hizo, Mhe. Rais Magufuli ameamua kuendesha harambee nyingine ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wa Waislamu wa Chamwino ambapo amefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi Milioni 48, mifuko 48 ya saruji na tripu 5 za mchanga kutoka kwa Waumini wa Parokia ya Bikira Maria Imakulata na Waumini wa Madhehebu mengine mbalimbali waliojitokeza papo hapo.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chamwino

23 Agosti, 2020

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi