Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli akutana na kuzungumza Prof. PLO Lumumba na Mwakilishi wa Kansela wa Ujerumani
Feb 24, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_51157" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli akisalimiana na Msomi na Mwanamajumui
(Pan-Africanist) kutoka Kenya Profesa Patrick Loch Otieno Lumumba (
Maarufu zaidi kama Profesa PLO Lumumba)
alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam
leo Jumatatu February 24. 2020[/caption]

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 24 Februari, 2020 amekutana na kufanya mazungumzo na Msomi na Mwanamajumui wa Afrika (Pan-Africanist) Prof. Patrick Loch Otieno Lumumba, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Magufuli na Prof. PLO Lumumba ambaye ni raia wa Kenya wamezungumzia masuala mbalimbali yahusuyo juhudi za Afrika katika kuimarisha uchumi kwa kutumia rasilimali zake na pia wajibu wa Waafrika na viongozi wao katika kuimarisha huduma za kijamii na kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Prof. PLO Lumumba kwa juhudi zake za kueleza waziwazi makosa yanayosababisha nchi za Afrika kubaki nyuma kiuchumi, kijamii na kisiasa, wajibu wa viongozi na wananchi wa Afrika katika kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi zao na mapenzi yake makubwa kwa Afrika.

Mhe. Rais Magufuli amemueleza juhudi ambazo Serikali ya Awamu ya Tano inazifanya katika kujenga uchumi imara wa kujitegemea ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway-SGR), ujenzi wa Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme, kuongeza usambazaji wa umeme kutoka vijiji 2,018 hadi kufikia vijiji 8,587, ujenzi wa barabara na madaraja makubwa na madogo, kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya elimu ya juu, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kudhibiti rasilimali muhimu ya madini na kupambana na rushwa.

[caption id="attachment_51150" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akipeana mikono naMwakilishi wa Kansela wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Afrika Bw. Guenter Nooke alipokutana na kufanya mazungumzo naye
Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu February 24. 2020[/caption]

“Mimi sijawahi kukutana nawe kabla, lakini nakusikia na kukuona kupitia vyombo vya habari jinsi unavyopaza sauti kuhusu Bara la Afrika, nakupongeza kwa juhudi hizo, na ninafarijika kwamba unaisemea vizuri Afrika” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Prof. PLO Lumumba amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutenga muda wake kuzungumza nae, na amempongeza kwa juhudi kubwa alizozionesha katika kipindi kifupi cha uongozi wake wa miaka 4 ambapo ameonesha mfano wa namna ya kupigania rasilimali za nchi ikiwemo madini, kujenga nidhamu ya utumishi Serikalini, kuimarisha uchumi, kupambana na wizi wa mali za umma, rushwa na ufisadi.

Prof. PLO Lumumba amesema inafaa kwa nchi za Afrika kujifunza mambo yanayofanyika Tanzania kwa sasa, na amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Waafrika kujiamini na kuchukua hatua madhubuti za kuwaondoa katika hali ya sasa ambapo rasilimali zake zinachukuliwa na Mataifa ya nje ilihali wananchi wake wakikabiliwa na changamoto mbalimbali.

[caption id="attachment_51153" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
katika picha ya pamoja Mwakilishi wa Kansela wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Afrika[/caption]

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Mwakilishi wa Kansela wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Afrika Bw. Guenter Nooke, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Bw. Nooke amewasilisha ujumbe wa Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel na pia ameelezea kufurahishwa kwake na hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa hapa nchini ikilinganishwa na alipokuja miaka iliyopita.

Pia amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi ambapo ameahidi kuwa Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji na biashara na masuala mengine ya kijamii.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Kansela wa Ujerumani kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kuuendeleza na kuukuza zaidi uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na Ujerumani, na inawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.

Katika mazungumzo hayo Bw. Nooke ameongoza na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe. Regine Hess.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

24 Februari, 2020

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi