Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Dkt. Magufuli Agawa Vitambulisho 670,000 kwa Wakuu wa Mikoa kwa Ajili ya Matumizi ya Wajasiriamali Wadogo Wadogo
Dec 11, 2018
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Fedha na Mipango kushirikiana na viongozi wa taasisi na vyombo mbalimbali vya umma kufanya tathmini ili kupata majawabu yatakayowezesha kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato hayo.

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 10 Desemba, 2018 wakati akizungumza katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa TRA wakiwemo Mameneja wa Mikoa yote nchini, Baadhi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa yote nchini, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Ofisi ya Takwimu ya Taifa, viongozi wakuu wa taasisi zinazohusika na udhibiti na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali nawajasiriamali wadogo kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais  Magufuli amesema mfumo na taratibu zinazotumika kukusanya mapato zina mapungufu makubwa hali iliyosababisha kuwepo kwa uwiano wa chini wa ukusanyaji wa kodi ikilinganishwa na nchi mbalimbali za Afrika, kutokuwepo kwa vyanzo vipya vya mapato, kutowavutia watu wengi kulipa kodi na kusababisha watu kufunga biashara zao.

Ameitaka TRA kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato na kuhamasisha zaidi watu kulipa kodi, kushirikiana na vyombo vya dola kubaini na kuwakamata wakwepa kodi wote hususani wanaosafirisha bidhaa mipakani kimagendo na kuacha kuwakatisha tamaa wafanyabiashara kwa kuwafanyia makadirio ya kodi kwa viwango cha juu visicholipika.

“TRA mnakwenda kwa mfanyabiashara mnamkadiria kodi shilingi Bilioni 2, anawaambia nitatoa Bilioni 1 au Milioni 800, mnakataa na mnaamua kumfungia biashara, sasa biashara ikifungwa utakuwa umepata nini? Tunashindwa hata kutumia busara zetu katika ukusanyaji wa kodi”amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewaonya baadhi ya viongozi wa siasa ambao wamekuwa wakiwakingia kifua wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi na amewaagiza maafisa wa TRA kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria bila kushinikizwa na mtu yeyote.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli ametoa vitambulisho vya wajasiriamali 670,000 kwa Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania (kila Mkuu wa Mkoa amekabidhiwa vitambulisho 25,000) kwa ajili ya kuwagawia wajasiriamali wa Mikoa hiyo ambao watavilipia shilingi 20,000 kwa kila kitambulisho kimoja, na ameagiza wajasiriamali watakaopatiwa vitambulisho hivyo wasibughudhiwe wakati wanafanya biashara zao.

“Mfanyabiashara mdogo akivaa kitambulisho hiki asisumbuliwe na mtu yeyote, na niseme kwa dhati ndugu zangu viongozi wa siasa mtu utakayemkuta na kitambulisho hiki na anafanya biashara ya chini ya Milioni 4 usimsumbue” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu kodi ya majengo Mhe. Rais Magufuli ameitaka TRA kuweka utaratibu rahisi wa kukusanya kodi ya majengo na ameelekeza nyumba ya kawaida iliyopo kijijini ilipiwe shilingi 10,000/= na nyumba ya ghorofa ilipiwe shilingi 20,000/=, kwa maeneo ya mjini nyumba ya kawaida ilipiwe shilingi 50,000/=, nyumba ya ghorofa kila sakafu ilipiwe shilingi 50,000/= na kodi itozwe kwa kiwanja na sio kila jengo lililopo katika kiwanja hicho.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa ametoa maelezo ya hali ya takwimu za kiuchumi hapa nchini na kubainisha kuwa takwimu za ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2018 zinaonesha kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa wastani mzuri wa asilimia 7.0 na mfumuko wa bei umeandika rekodi ya chini zaidi kuwahi kutokea katika miaka 10 ambapo ilikuwa wastani wa asilimia 3.0 katika mwezi Novemba 2018.

Nae Gavana wa BOT Prof. Florens Luoga amesema benki hiyo imeendelea kufanya juhudi za kusimamia na kuimarisha sekta ya fedha ambapo ukopeshaji kutoka benki mbalimbali kwenye kwa wafanyabiashara umepanda kutoka asilimia 0.8 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 4.9 Septemba 2018, BOT imepunguza riba kwa mikopo yake kwa benki kutoka asilimia 16-12 mwaka 2017, kutoka asilimia 12 hadi asilimia 7 mwaka 2018 na kwamba inaelekea kufikia asilimia 3.5.

Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere ameeleza juhudi mbalimbali za kuongeza ukusanyaji wa mapato zilizofanikisha kukusanya shilingi Trilioni 42.9 katika kipindi cha miaka 3 iliyopita na kwamba hivi sasa inaendelea kuimarisha mifumo hususani bandarini ambapo mfanyabiashara atapata huduma kwa pamoja.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango ameahidi kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli na ameagiza maafisa masuhuli wote kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinaingizwa katika mfuko mkuu wa Serikali pamoja na kuhakikisha hawaingii mikataba mipya ya misamaha ya kodi bila kupata ridhaa ya Waziri wa Fedha na Mipango.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasilinao ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

10 Desemba, 2018

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi