Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika Kusini zaridhia kutekeleza Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika.
Makubaliano hayo yamefanyika tarehe 19/09/2017 baina ya Tanzania na Afrika Kusini yakiwahusisha Mawaziri wenye dhamana ya Utamaduni kutoka nchi hizo pamoja na Mawaziri kutoka Wizara za kisekta zinazohusika na utekelezaji wa Programu hiyo.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Tanzania ina mchango wa hali na mali katika harakati za ukombozi wa nchi za Bara la Afrika pamoja na uanzishwaji wa program hiyo inayolenga kuhifadhi Urithi huo kwa kushirikiana na wadau.
“ Mwaka 2002 programu hiyo iliridhiwa na Mkutano Mkuu wa 33 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU) wa mwezi Januari, 2011” ameongeza Dkt. Mwakyembe.
Aidha, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa, moja ya makubalino ni kuendeleza jitihada za kufanya tafiti zaidi baada ya kukamilika kwa utafiti wa Mradi wa Hashimu Mbita na kufanya juhudi za makusudi kuorodhesha nyaraka za iliyokuwa Kamati ya Ukombozi wa Bara la Afrika katika kumbukumbu ya Dunia.
Kwa upande wake Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini Nathi Mthethwa amesema kuwa Programu hiyo itaimarisha ushirikiano katika kuongeza idadi ya maeneo ya Urithi wa Dunia yanayohusiana na Harakati za Ukombozi yanaorodheshwa kwa pamoja baia ya nchi moja na nyingine hususani Urithi wa Ukombozi usioshikika.
“Kuna baadhi ya vizazi havielewi machungu ya kutawaliwa, hivyo nashauri mifumo ya elimu katika nchi za Afrika izingatie masuala ya ukombozi wa Bara la Afrika ili kuleta uelewa kwa kizazi kilichopo na vizazi vijavyo” ameongeza Mhe. Mthethwa.
Programu hiyo ina wajibu wa kukusanya, kuweka kumbukumbu, kuhifadhi na kukumbuka nakishi ya Urithi wa Afrika tangu harakati za kupigania Uhuru wa Afrika hadi Bara zima lilipokombolewa.
MWISHO