Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Prof, Mbarawa Aitaka Bodi Mpya ya TTCL Kujipanga
Sep 21, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_14746" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo mbele ya wajumbe wa Bodi ya Kampuni ya Simu ya TTCL katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Omary Nundu.[/caption]

Thobias Robert

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Mkame Mbarawa ameitaka Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya kampuni ya mawasiliano nchini (TTCL) kuhakikisha kuwa inasimamia vyema kazi na majukumu yake ili kuiwezesha kampuni hiyo kujiendesha kibiashara na kuimarisha huduma za mawasiliano hapa nchini.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi  wa bodi hiyo ambapo aliwasisistiza kuwa wachape kazi ili kurahisisha huduma mbalimbali za kimawasiliano hapa nchini na kuhakikisha kuwa wanaendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano yenye sera ya hapa kazi tu.

[caption id="attachment_14747" align="aligncenter" width="750"] Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Simu za Mkononi ya TTCL Mhandisi, Omary Nundu akielezea jambo wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo.[/caption]

“Nataka bodi mjue tunakwenda wapi katika kampuni hii lakini pia tunahitaji kufanya kazi kwa juhudi, kushindana na makampuni mengine ya simu, mhakikishe mapato makubwa yanatoka kwenye data  halikadhalika tujue mnapaswa mjue strenght (nguvu) yenu iko wapi maana tusipojibu maswali haya hatuwezi kufanya ushindani na makampuni mengine,” alifafanua Prof. Mbarawa.

Aidha Prof. Mbarawa alisema kuwa, Serikali imeweka sera nzuri za uwekezaji katika sekta ya mawasiliano kiasi ambacho kimeongeza mapato pamoja na ushindani wa huduma ya mawasiliano na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo hapa nchini.

[caption id="attachment_14749" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi ya Kampuni ya Simu ya Mkononi ya TTCL leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TTCL, Bw. Waziri Kindamba, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Mhandisi Omary Nundu na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.[/caption]

Prof. Mbarawa aliongeza kuwa serikali imefanya mabadiliko yaliyofanywa na serikali ili kuipa nguvu Kampuni ya TTCL ikiwa ni pamoja na kuondoa ubia wa umiliki wa TTCL na wawekezaji asilimia 35 na kuzirejesha serikalini, kujenga mkongo wa taifa wa mawasilino, kujenga kituo cha taifa cha kuhifadhi kumbukumbu (Data center) pamoja na kulipa madeni ya kampuni hiyo.

Aidha Prof. Mbarawa ameitaka Bodi ya Wakurugenzi kuhakiksha kuwa TTCL inaleta mabadliko na maendeleo katika kufikia sera ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda, kuongeza wateja na watumiaji wa huduma zitokanazo na TTCL, kuwafikia watumiaji wengi zaidi nchini kote na kuendelea kuwa kampuni bora ya mawasiliano.

Prof. Mbarawa aliongeza kuwa, TTCL ni lazima wabadilike katika utoaji wa huduma zake, ili kuendana na manadiliko ya teknolojia ambapo amewaeleza kuwa kwenye sekta ya mawasiliano mambo yanabadilika kila siku, sekta inakua haraka na hata uendeshaji wake unabadilika.

[caption id="attachment_14752" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya TTCL wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na: Frank Shija)[/caption]

“Mathalani ukiangalia makampuni makubwa kwa sasa, mapato yao yamebadilika kutoka kwenye sauti hadi data pamoja na miamala ya pesa hivyo TTCL wanapaswa wajipime waangalie uwezo wao uko wapi na nguvu zao ziko wapi ili waweze kujipanga vizuri kuhakikisha wanashindana na makampuni mengine ya mawasiliano hapa nchini,” alifafanua Prof. Mbarawa.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Mhandisi Omary Nundu, alisema kuwa tangu ateuliwe katika bodi hiyo mambo mengi wameyafanya hadi  sasa ikiwemo kuifufua kampuni hiyo, kushirikiana na wadau wengine wa mawasiliano pamoja na  kuanzisha TTCL Pesa.

“Kwa sasa tunahudumia watu laki tatu hapa nchini, lakini tumenuia mwisho wa mwaka huu wa fedha 2017/2018 tufikie wateja milioni moja na baada ya miaka mitano yaani ifikapo 2021/2022 tuwe na wateja milioni tano ambapo tutakuwa tumefikia asilimia 10 ya wateja wa soko la mawasiliano hapa nchini,” alifafanua Mhandisi Nundu.

Aidha, Mhandisi Nundu aliendelea kusema kuwa mwaka 2016, TTCL ilipata bilioni 0.21 katika soko lake na zaidi mwaka huu wanatarajia kupata bilioni 0.3 na kwamba wanatarajia kupata faida ya zaidi ya bilioni 40 ifikapo 2022 baada ya makato ya kodi.

“Katika kuyafanikisha matarajio yote haya, tunapaswa kupata jumla ya dola za kimarekani  milioni 673,  ambapo dola milioni 300 tunatarajia kuzipata kama mtaji wa uwekezaji kutoka serikalini, huku kampuni ikitafuta njia nyingine za kuapata fedha zilizobaki katika mpango na matarajio yetu,” alifafanua Mhandisi Nundu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Mawasiliano Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Maria Sasabo alisema sekta ya mawasiliano ni kiungo muhimu katika kukuza uchumi kwa kurahisisha mawasiliano ya kati ya mtu na mtu na taifa kwa ujumla kwa kurahisisha usambazaji na upatikanaji wa huduma na bidhaa kutoka sehemu moja na nyingine.

“Sera ya serikali ya kuelekea uchumi wa viwanda inatoa fursa kubwa kwa sekta ya mawasiliano kukua, pia ukuaji wa shughuli za uchumi unachochea mahitaji ya mawasiliano kuongezeka ikiwemo serikali mtandao, tiba mtandao, elimu mtandao, biashara mtandao, utangazaji mtandao kwa njia ya runinga na radi,” alifafanua Dkt.Sasabo.

Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL iliteuliwa rasmi mwezi Februari 2017,na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni jitihada za kufufua na kurejesha kampuni hiyo katika ushindani, kusimamia mawasiliano yote ya serikali na kujiendesha kwa faida. Kwa sasa serikali inajiandaa kupeleka muswada bungeni ili  kuirasimisha TCCL  iwe na bajeti ya kujitegemea.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi