Na: Frank Mvungi – MAELEZO, Dodoma
Kuimarika kwa Mawasiliano Kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri kumetajwa kuwa chachu ya kuboreshwa kwa huduma za jamii hasa kupitia kwa mfumo mpya wa kielektroniki utakaowezesha wananchi kushiriki katika Kupanga na kuamua vipaumbele vyao katika sekta zinazogusa maisha yao kila siku ikiwemo Afya.
Akizungumza katika mahojiano maalum Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Asha Mahita ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafumzo ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki utakaotumika kuandaa Bajeti,Mipango na Kutoa ripoti alisema kuwa ni chachu kwa watendaji wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kwa kuwa wataweza kujipima na kufanya tathmini wao wenyewe kupitia mfumo huo kulingana na malengo yaliyowekwa
“Lazima sasa kila mtu afanye kazi kwa juhudi na kujituma kwa kuwa mfumo umeainisha kila jukumu na mtekelezaji wake hali itakayosaidia kuongeza uwajibikaji katika maeneo ya kutolea huduma kama Zahanati, Shule na Vituo vya Afya.” Alisisistiza Dkt. Mahita
Akifafanua Dkt. Mahita amesema kuwa mfumo huo unawawezesha watendaji kufanya uchambuzi wa Bajeti kabla ya kuiwasilisha katika ngazi husika kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Dkt. Frank Chiduo amesema kuwa kupitia mfumo wa PlanRep iliyoboreshwa kutakuwa na uwazi na uwajibikaji wa pamoja unaozingatia hali halisi ya wananchi wanaopata huduma katika vituo vya kutolea huduma.
“ Muda uliokuwa unatumika kuandaa bajeti na Mipango sasa utapungua kwa kiasi kikubwa hivyo kuwapa nafasi watendaji wa Serikali kutatua changamoto zilizojitokeza katika kuwahudumia wananchi,” alisisitiza Dkt. Chiduo.
Mradi wa PS3 umejikita katika maeneo makuu matano ambayo ni Utawala Bora na Ushirikishwaji wananchi, Rasilimali watu, Rasilimali Fedha, Mifumo ya TEHAMA pamoja na Tafiti Tendaji, Tathimini na ufuatiliaji.
Mafunzo kwa watumiaji wa mfumo wa PlanRep tayari yamefanyika katika Mikoa ya Mtwara, Morogoro, Mbeya, Mwanza, Kigoma na sasa Dodoma.Washiriki wa mafunzo hayo ni Waganga wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wachumi, Maafisa TEHAMA, Maafisa Mipango, na Wahasibu.