Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ofisi ya Makamu wa Rais Yasaini Mkataba Ujenzi na Ukarabati wa Kingo za Fukwe
Mar 31, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Ofisi ya Makamu wa Rais na Kampuni ya Ujenzi ya DEZO Civil Contractors Co. Ltd. zimesaini mkataba wa ujenzi na ukarabati wa kingo za fukwe katika maeneo ya mwambao wa Mikindani (Mtwara) wenye urefu wa mita 1,750 na Sipwese (Pemba) mita 500 wenye thamani ya shilingi. bilioni 4.4 ambao utagharamiwa na Serikali ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa ujenzi huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga alionesha imani kuwa mradi huo utamalizika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.

Alimtaka mkandarasi kuzingatia viwango vya ubora wakati wa ujenzi wa mradi huo ili uweze kuleta manufaa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi hususan katika mmomonyoko wa fukwe nchini.

“Tumewaamini mtafanya kazi vizuri na msituangushe, tuna imani mtazingatia thamani ya fedha mlizotengewa katika kujenga mradi huu hivyo nawatakia kila la heri mkamilishe kwa wakati,” alisema Bi. Maganga.

Aliongeza kuwa maeneo mengi yameharibiwa kutokana na maji ya bahari kuingia nchi kavu na hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo inasimamia mazingira inatekeleza miradi ya kukabiliana na changamoto hizi katika maeneo ya pwani.

Katibu Mkuu huyo alisema kuwa mbali ya mradi huo pia kuna miradi mingine mikubwa ambayo tayari imejengwa ikiwemo ukuta kwenye Barabara ya Barack Obama jijini Dar es Salaam ambao unasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Dezo Civil Contractors Co. Ltd, Bw. Premji Pindoria aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuiamini kampuni hiyo na kuahidi kumaliza mradi huo kwa wakati.

Alisema watatumia uzoefu na utaaamu wao kama walionesha katika ujenzi wa wa kuta za Barack Obama, Chuo cha Mwalimu Nyerere Kigamboni (Dar es Salaam), Pangani mkoani Tanga na visiwa Panza (Pemba).

Aidha, mmomonyoko huo umekuwa ukisababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara, mashamba na makazi ya watu hivyo mradi huo unatarajiwa kuwa suluhu. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 18.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi