[caption id="attachment_46958" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kabeho wilayani Chato, alipofika kuwawashia rasmi umeme, Septemba 16, 2019.[/caption]
Na Veronica Simba - Geita
Serikali imewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuwaunganishia umeme wananchi wa vijiji vyote 11 vya Kata ya Nyankumbu iliyopo Geita mjini, kwa gharama ya shilingi 27,000 tu kuanzia sasa.
Agizo hilo lilitolewa jana, Septemba 16 mwaka huu na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, wakati akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Uwanja, Kata ya Nyankumbu, akiwa katika ziara ya kazi.
Waziri alisema, awali, Kata hiyo haikuwa katika mpango wa umeme vijijini, ambao wanufaika wake ndiyo huunganishiwa umeme kwa gharama hiyo lakini baada ya serikali kujiridhisha kuwa eneo hilo halina tofauti na maeneo mengi ya vijijini, imeamua nao wapatiwe huduma hiyo kwa gharama inayotozwa vijijini.
[caption id="attachment_46959" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), akimkabidhi kifaa cha Umeme Tayari (UMETA), mmoja wa wanakijiji wa Kabeho wilayani Chato, wakati wa hafla ya uwashaji rasmi umeme katika kijiji hicho.[/caption]Aidha, Waziri aliwaagiza viongozi wa taasisi husika kwa kushirikiana na mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini, awamu ya tatu, wilayani humo, kuweka magenge 10 katika Kata hiyo na waanze kuunganishia wananchi umeme mara moja.
Hata hivyo, Waziri Kalemani alibainisha kuwa, watakaounganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 katika eneo hilo, ni wale tu wateja wapya na kwamba wale ambao walikwishaunganishiwa awali kwa gharama tofauti, hawatahusika na hawatarejeshewa fedha.
Katika hatua nyingine, Waziri aliendelea kusisitiza agizo lililotolewa na serikali kuwa wananchi vijijini hawapaswi kulipia nguzo wala kifaa kingine chochote isipokuwa gharama za kutandaza mfumo wa nyaya kwenye majengo yao (wiring), ambazo ni makubaliano yao binafsi na wakandarasi watakaowafanyia kazi hiyo.
[caption id="attachment_46960" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akikata utepe kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika Shule ya Msingi ya Kabeho, iliyopo wilayani Chato.[/caption]Alitoa onyo kali kwa yeyote atakayebainika kumwambia mwananchi kulipia nguzo au kumtoza gharama nyingine yoyote zaidi ya shilingi 27,000 tu ambayo ndiyo bei halali iliyotangazwa na serikali kwa ajili ya kuunganishia umeme wananchi wa vijijini.
Katika ziara hiyo, Waziri pia alitembelea kijiji cha Kabeho kilichopo wilayani Chato mkoani humo, ambapo aliwasha rasmi umeme katika Shule ya Msingi ya kijiji hicho.
Aliwataka wanafunzi kuutumia umeme huo kwa ajili ya kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni hapo.