[caption id="attachment_42289" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Wiaya ya Tunduru, Juma Homera akisisitiza jambo (Picha na Maktaba)[/caption]
Na: Theresia Mallya, Tunduru DC
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Juma Zuberi Homera amesema kuwa ni wajibu kwa kila kiongozi kusikiliza na kutatua kero za wananchi ili kufikia maendeleo endelevu kama ilivyo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano. Mhe. Homera ameyasema hayo wakati wa ziara kukagua mashamba ya Ufuta, kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Tarafa za Namasakata na Lukumbule zilizopo katika jimbo la Tunduru Kusini.Akifafanua, amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Help for Underserved Community (H.U.C) wanachimba visima vya maji katika majimbo yote mawili ya Tunduru Kusini na Kaskazini ili kupunguza tatizo la maji katika Halmashauri ya Tunduru.
Mhe. Homera aliendelea kusema kuwa jumla ya visima 125 kwa michango ya wananchi pamoja na mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo katika vijiji 60 vya Wilaya ya Tunduru, vimechimbwa ambapo visima 57 vimekamilika na vinatoa huduma kwa wananchi.
Aidha, Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Help for Underserved Community (H.U.C) kwa sasa inaendelea kufanya utafiti katika vijiji vilivyosalia ili kufanya uchimbaji wa visima vya maji vilivyosalia kuanzia mwezi Mei 2019.
Ambapo vitachimbwa visima 11 katika Kata ya Tuwemacho, viwili viwili katika vijiji vya Nasya, Namasalau na Chemchemi, na visima vitano kijiji cha Tuwemacho ambapo visima vitatu ni mchango wa Mkuu wa Wilaya na visima viwili mchango wa mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo la Tunduru Kusini.
Mhe. Homera aliendelea kusema kuwa ili kuongeza uzalishaji na wananchi kufanya kazi za kujiletea maendeleo ni vyema huduma za jamii kama maji kuwepo karibu , ili kufikia lengo la serikali la upatikanaji wa maji vijijini kwa asilimia 85 ifikapo 2020.
Hata hivyo upatikanaji wa maji safi na salama katika Halmashauri ya Tunduru hadi kufikia Aprili 2019 ni asilimia 69 kwa maji mjini na asilimia 68.5 maji vijijini.