Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

NHIF Yachangia Mageuzi Sekta ya Afya Nchini
Apr 05, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Frank Mvungi

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetajwa  kuchochea  mageuzi  katika ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya hapa nchini hali ilichangia kupungua kwa idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kupata matibabu.

Akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF  Bw. Benard Konga amesema kuwa uwekezaji  mkubwa umefanywa na mfuko huo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI),  KCMC, Bugando na Hospitali za Kanda kwa kuchangia kuimarisha huduma za kibingwa na miundombinu kama majengo.

Aliongeza kuwa matibabu ya kibingwa kama ya upandikizaji figo yanafanyika hapa nchini  kwa sasa kutokana na juhudi za  kuimarisha huduma za afya zinazofanywa na Serikali kupitia NHIF.

“ Vituo zaidi ya 7000 vimesajiliwa kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF kote nchini ambapo mafao mbalimbali yameanzishwa ikiwemo linalowawezesha wakulima kupata huduma hizi kupitia vyama vyao vya ushirika na tumenza na wale walio katika uzalishaji wa mazao ya kimkakati kama pamba, kahawa, korosho, chikichi na alizeti,” alisisitiza Konga

Akifafanua, amesema kuwa moja ya mikakati ya NHIF kusogeza huduma kwa wananchi imekuwa kutekeleza programu ya kupeleka madaktari bingwa katika mikoa ya pembezoni ambayo ina upungufu wa wataalamu hao ambapo wagonjwa 21,375 wamehudumiwa kupitia utaratibu huu na kati yao 1,020 wakifanyiwa upasuaji wa aina mbalimbali.

Aliongeza kuwa mfuko huo kwa kushirikiana na Benki ya Watu wa Ujerumani (KfW) inatekeleza mpango wa tumaini la mama katika mikoa ya Tanga, Lindi, Mtwara, Mbeya  na Songwe ili kusaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.

“Hadi Juni 2018 vituo takribani 330 vimeshaomba na kuidhinishiwa mikopo ya vifaa tiba kama MRI, CT SCAN ambapo mikopo hiyo imeshaidhinishwa na kuchangia katika kuleta mageuzi sekta ya afya hapa nchini kutokana na kuimarika kwa huduma za afya kwa wananchi,” alisisitiza Konga

Aidha, Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi wa Viwanda, NHIF  kwa kushirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na wadau mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Mkoa wa Simiyu inatekeleza uwekezaji wa ujenzi wa kiwanda kitakachozalisha bidhaa mbalimbali za hospitali zitokanazo na malighafi pamba.

Watanzania asilimia 32 wananufaika na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na kati ya hao asilimia 25 ni wale wanaonufaika kupata matibabu kupitia Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF)  ambapo mpango ni kufikia asilimia 50 ya Watanzania ifikapo mwaka 2020.

Mfuko wa Taifa  wa Bima ya Afya umejidhatiti kuendelea kuchangia katika kuboresha huduma za afya hapa nchini na kusaidia kuchangia katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi ili waweze kushiriki katika ujenzi wa Taifa na uchumi wa viwanda.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi