Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Serikali imeagiza Menejimenti ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kubuni na kutekeleza mikakati ya kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujiunga na kunufaika na Mfuko huo ili kufikia adhma ya Serikali ya Afya Bora kwa wote.
Wakati huo huo, Serikali imezionya Hospitali zote nchini kuacha mara moja kufanya udanganyifu katika madai ya malipo yatokanayo na huduma wanazozitoa kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Godwin Mollel wakati akizungumza na Menejimenti ya NHIF na Waandishi wa Habari mjini Morogoro kuhusiana na uboreshaji wa huduma za NHIF kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
“Nawapongeza mmeweka utaratibu wa kila mwananchi kuweza kujiunga lakini ongezeni jitihada katika kuwafikia wananchi waliko ili waweze kujiunga na kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu, Serikali itaendelea kuulea Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili uimarike na kuendelea kupanua wigo na ubora wa huduma kwa wananchi wote, hivyo natoa onyo kwa vituo vinavyojihusisha na udhanganyifu wowote,” alisema Dkt. Mollel.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi ambapo mikakati hiyo ni pamoja na pamoja na kuongeza bajeti ya dawa kutoka bilioni 30 mwaka 2015 hadi kufikia bilioni 270.
“Tumeona uboreshaji wa miundombinu ya huduma za Hospitali ikiwemo ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na Hospitali za Rufaa za Mkoa, kuongeza Madaktari katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi za chini na kuongeza vifaa tiba na vitendanishi ili kuwezesha wananchi wengi kupata huduma karibu na maeneo wanayoishi, haya ni mafanikio makubwa ambayo yameonekana” alisema Mhe. Naibu Waziri.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wananchi na huduma zitolewazo na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekutana na Viongozi waandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na MSD kwa lengo la kupanga mikakati ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hizo.
Kutokana na kikao hicho, Serikali imefanya maboresho katika orodha ya Taifa ya Dawa muhimu kwa kuongeza aina ya dawa 71 ambazo hazikuwepo awali ambapo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya tayari umeongeza dawa hizo katika kitita chake cha mafao kitolewacho kwa wanufaika wake.
“Tumeuelekeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuwasilisha maboresho ya kitita cha huduma zitolewazo kwa wanachama kwa ajili ya maamuzi na kuanza kutumika; Kufanya mapitio ya utaratibu wa mikopo itolewayo kwa watoa huduma ikiwemo ya dawa, ukarabati wa vituo, vifaa tiba na vitendanishi ili kuongeza tija na kupunguza gharama,” alisema.
Katika kikao hicho, Naibu Waziri huyo aliongozana na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi na Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Brig. Jen Dkt. Gabriel Sauli Mhidize.