[caption id="attachment_46998" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akiwasha umeme katika Kijiji cha Mlamleni wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani.[/caption]
Na Hafsa Omar, Pwani
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ameendelea kukagua utekelezaji wa kazi ya kusambaza umeme vijijini pamoja na kuwasha umeme katika vijiji mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa vijiji vyote vinafikiwa na nishati ya umeme ifikapo mwaka 2021.
Tarehe 16 Septemba, 2019, alikagua kazi ya usambazaji umeme katika vitongoji vya Kisasa na Churwi pamoja na kuwasha umeme katika kijiji cha Mlamleni Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani .
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mlamleni, Naibu Waziri alieleza kuwa wakandarasi wakikamilisha miradi ya umeme na kukabidhi kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wananchi wataunganishiwa kwa bei ile ile ya shilingi 27,000.
[caption id="attachment_47000" align="aligncenter" width="640"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa vitongoji vya Kisasa na Churwi mara baada ya kufika katika Vitongoji hivyo kukagua kazi ya usambazaji umeme.[/caption]Aliwaahidi wananchi wa kijiji hicho kuwa, umeme utasambazwa kwa wananchi wote kwani Tanesco inahitaji wateja ili Shirika hilo liweze kujiendesha lenyewe, hivyo ni lazima wateja wengi wapatikane.
Naibu waziri alisema kuwa, Wilaya ya Mkuranga ni moja ya wilaya ambazo zipo kwenye mradi wa umeme wa ujazilizi awamu ya pili (A) utakaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo maeneo mengi zaidi yataunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000.
Vilevile, alisema kuwa, wilaya hiyo itasambaziwa umeme kupitia mradi wa Peri-Urban ambapo wananchi 4293 ambao ni wateja wa awali wataunganishwa.