Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutoa kitalu cha Uwindaji wa Kitalii kwa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka ili kitumike kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosomea masomo ya Uwindaji Bingwa (Professional Hunters)
Ametoa agizo hilo leo wakati akizindua Bodi ya Magavana ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilichopo katika wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mhe. Kanyasu amesema kitalu hicho cha uwindaji wa kitalii kitakisaidia chuo hicho kuzalisha wataalamu wenye sifa.
Amesema kwa sasa Mabingwa wa Uwindaji wa Kitalii wanaofanya kazi hiyo hapa nchini ni raia wa kigeni na baadhi ya Wazawa waliopo ni Wazee.
Amesema kitalu hicho kitachochea kupata Wataalamu wa kutosha ili kuweza kukabiliana na uhaba wa Wataalamu wa fani hiyo.
Aidha, Mhe. Kanyasu amesema chuo hicho kitasaidia kukabiliana na Wafugaji wanaoingiza vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa vile vitalu vingi bado vipo wazi hali inayopelekea Wafugaji wengi kuingiza mifugo hivyo.
Pia, Amesema Kitalu hicho hakitasaidia Wahitimu pekee kufanya mafunzo kwa vitendo bali itasaidia Wanyamapori kuwa salama kwa sababu chuo hicho kitakuwa na jukumu la kupambana na tatizo la ujangili.
Aidha, Mhe. Kanyasu amempongeza Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Faustine Bee kwa kuchaguliwa kwa awamu ya pili kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo pamoja na Magavana wa Bodi kwa asilimia kubwa kuteuliwa tena kuendelea kukitumia chuo hicho.
Awali, Mkuu wa chuo hicho, Prof. Jaffari Kidegesho amesema kwa sasa wanafunzi wa chuo hicho wamekosa maeneo ya kufanyia mafunzo kwa vitendo kwa ajili ya uwindaji wa kitalii.
Amesema mwanzo chuo hicho kilikuwa kikiyatumia mapori ya Akiba kwa ajili ya mafunzo hayo ila kwa sasa mapori hayo yamepandishwa hadhi na kuwa Hifadhi za Taifa hivyo katika Hifadhi hizo hakuna shughuli za kibindamu zinazoruhusiwa kufanyika kwa mujibu wa sheria.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori, Mweka, Prof. Jaffari Kidegesho amesema kitalu hicho kitasaidia kufanya mafunzo kwa vitendo na hivyo kutasaidia kuwaandaa wahitimu wenye sifa kulingana na mahitaji ya soko
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki amekitaka Chuo hicho kuboresha mtaala wa mafunzo hayo ili kuzalisha Wataalamu wataoweza kujibu changamoto za soko.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilimanjaro, Alhaji Rajabu Kundya amesema suala la uhifadhi na utalii limekuwa na mchango mkubwa sana kwa uchumi wa Taifa hali iliyopelekea Tanzania kuwa na Uchumi.
Amesema shughuli hizo wanazichukulia kwa uzito mkubwa na wanakithamini sana chuo hicho kwa mchango mkubwa wa kuzalisha wasomi wenye weledi.
Itakumbukwa kuwa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka ndo chuo pekee nchini kinachotoa mafunzo ya Uwindaji Bingwa wa Kitalii (PH)