Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Kandege Afurahishwa na Miradi ya TARURA – Ilemela.
Feb 26, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_51207" align="aligncenter" width="750"] Muonekano wa Barabara ya Sabasaba - Kiseke - Buswelu iliyojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini- TARURA Ilemela Jijini Mwanza.[/caption]

Na, Geofrey Kazaula

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Josephat Kandege ameelezea kuridhishwa kwake na miradi ya barabara iliyotekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)  katika Manispaa ya Ilemela Jijini Mwanza.

Aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Mwanza ambapo ameeleza kuwa mafanikio yanayopatikana katika Manispaa  hiyo hasa katika miradi ya barabara yanatokana na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya wataalam wa TARURA  na watumishi wengine wa Manispaa kwa kufanya kazi pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi.

‘‘Wote tumeshuhudia barabara hizi zilivyo kwenye kiwango, mafanikio haya yanatokana na umoja uliopo kwa watumishi wote wa Manispaa ya Ilemela pamoja na watumishi wa TARURA  kwani wanafanya kazi kwa pamoja ili kuwaletea wananchi wetu maendeleo, kiujumla wanafanya vizuri’’, alisema Kandege.

Aidha, amesisitiza kuwa miundombinu ya barabara inapokamilika ilindwe kwa nguvu zote na amewaagiza viongozi husika huhakikisha barabara hizo zinafanyiwa usafi mara kwa mara na kulinda miundombinu ya barabara hizo.

Naye Meneja wa TARURA Manispaa ya Ilemela, Mhandisi Clement Kihinga amesema kuwa barabara hizo zilizotekelezwa chini ya mradi wa Tanzania Strategic Cities Project (TSP) zimekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuinua uchumi wa wananchi na kuboresha kiwango cha maisha ya wananchi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanailinda miundombinu ya barabara ili idumu na iendelee kuboresha maisha yao na kurahisisha suala la usafiri na usafirishaji katika Manispaa ya Ilemela.

‘‘Serikali inatumia gharama kubwa sana kujenga barabara hizi hivyo nitoe wito kwa wananchi kuhakikisha kila mmoja wetu anashiriki kulinda miundombinu hii ya barabara ’’, alisema Mtaalam huyo.

Mmoja wa wananchi wa Kiseke A Ilemela, Issa Shabani alisema awali usafiri ulikuwa changamoto sana Katika barabara yao kwani miundombinu ilikuwa mibovu sana ila baada ya barabara ya kiseke Busweru kukamilika maisha yamepanda kiuchumi.

“Sasa nafanya biashara yangu ya matunda hapa Busweru, nayabeba salama na hayaharibiki kwani barabara ni nzuri na hata kipato changu kimeongezeka hivyo naishukuru sana Serikali kwa kujenga barabara hii”, alisema Shabani

Ziara ya Mhe. Kandege inaendelea mkoani Mwanza ambapo miradi mbalibali ya maendeleo zikiwemo barabara zinazosimamiwa na TARURA inatarajiwa kukaguliwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi