Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Akizungumza leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, alisema kuwa wa sasa juhudi kubwa zimeelekezwa katika kuongeza uzalishaji katika viwanda vya sukari vilivyopo Kagera, Mtibwa na Kilombero pamoja na kuhamasisha kuanzishwa kwa mashamba na viwanda vipya vitakavyozalisha sukari nchini.
Msigwa alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo viwanda vya sukari vya Kagera, Mtibwa na Kilombero vinatarajia kuongeza uzalishaji wa tani 265,000, ambazo zitaongezeka kwenye tani 367,000 zinazozalishwa sasa.
Alibainisha kuwa wawekezaji wapya wa Bagamoyo Sugar wameshalima shamba na tayari wamefunga mitambo Bagamoyo mkoani Pwani ambapo wanatarajia kuzalisha sukari kuanzia mwezi Juni mwaka 2022 wakianza na tani 20,000 na baadaye kuzalisha zaidi ya tani 50,000 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Aidha, mradi wa uwekezaji wa ubia kati ya NSSF na Magereza Mbigiri (Mkulazi 2) shamba limeshalimwa na uzalishaji unatarajiwa kuanza kati ya Julai na Agosti mwaka 2022 kwa kuzalisha tani 50,000.
“Ukijulimlisha haya yote katika kipindi cha miaka mitatu ijayo tunatarajia kuwa na uzalishaji mpya wa sukari wa jumla ya tani 305,000 ambazo zitaungana na tani za sasa 367,000. Kwa hiyo katika miaka mitatu ijayo tunatarajia uzalishaji wa jumla ya tani 672,000, huu utakuwa ni uzalishaji mkubwa ukilinganishwa na mahitaji ya nchi kwa sasa ya tani 420,000 na sukari ya viwandani ya tani 150,000.” Alisisitiza Msigwa
Vilevile, Msigwa alisema kuwa kwa wakati huu ambapo kuna upungufu wa sukari ambao nchi hupata kati ya mwezi Aprili na Juni Serikali imeamua kiasi cha sukari inayopungua katika mahitaji ya nchi iagizwe na wamiliki wa viwanda vya kuzalisha sukari kwa makubaliano ya kuongeza uzalishaji katika mashamba na viwanda vyao.
Serikali inawahakikishia wananchi kuwa itaendelea kuhakikisha Watanzania wanapata sukari, ambayo ni salama na kwa bei nafuu. Na kwamba sio muda mrefu kutakuwa na sukari ya kutosha inayozalishwa hapa hapa nchini.