Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mtandao wa DART kufikishwa Mkuranga, Bagamoyo na Kisarawe
Aug 07, 2026
Mtandao wa DART kufikishwa Mkuranga, Bagamoyo na Kisarawe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, afungua Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka, Awamu ya Pili (BRT II) katika Barabara ya Kilwa, Chang’ombe, Sokoine na Kawawa, Jijini Dar es Salaam.
Na Baraka Messa – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kupanua mtandao wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) hadi Mkuranga, Bagamoyo na Kisarawe ikiwa ni hatua ya kuboresha huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo, Agost 7,2026 Dkt. Samia amewapongeza wananchi wa Dar es Salaam kwa uvumilivu walioonyesha wakati wa ujenzi wa miundombinu hiyo, akisema walivumilia vumbi, foleni na usumbufu mwingi ambao sasa umeanza kuzaa matunda kupitia huduma bora ya usafiri.

Amesema uwekezaji huo umefanyika kutokana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam, ambapo huduma ya mabasi yaendayo haraka imepunguza muda wa safari kutoka zaidi ya saa moja na nusu hadi takribani dakika 30, huku ikiongeza  uwezo wa kuhudumia abiria wengi zaidi, kupunguza foleni na kuibua fursa za ajira kwa vijana.

"Nimezielekeza Wizara ya Ujenzi, TAMISEMI na taasisi zote zinazohusika kuhakikisha miradi ya barabara inakamilika kwa wakati. Pia DART iongeze mabasi katika maeneo yenye mahitaji makubwa ili wananchi wapate huduma kwa haraka zaidi," amesema Rais Samia.

Aidha, amewataka Watanzania, hususan vijana, kulinda miundombinu ya umma, akisisitiza kuwa uharibifu wa miundombinu hiyo unarudisha nyuma maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega amesema mradi huo umefuta changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili wakazi wa Mbagala na maeneo ya Temeke kwa miaka mingi.

Ulega amebainisha kuwa yeye akiwa mzaliwa wa Temeke na kukulia Mbagala, anashuhudia kuwa wananchi wa eneo hilo walikuwa wakipitia mateso makubwa ya usafiri, wakigombea mabasi na wakati mwingine kutembea umbali mrefu ili kufika makazini au nyumbani.

Amesema kabla ya mradi huo, wakazi wengi wa Mbagala walilazimika kulipa nauli mara mbili kila siku kufika Kariakoo au Posta, hali iliyowaongezea mzigo wa maisha, hasa kwa wamachinga na wafanyabiashara wadogo.

"Kupungua kwa gharama na muda wa usafiri kupitia mradi huu wa mwendokasi kutawaongezea wananchi fursa za kufanya kazi, kufanya biashara na kuboresha maisha yao," amesema Ulega.

Upanuzi wa mtandao wa DART pamoja na kuimarishwa kwa huduma zake utachochea maendeleo ya kiuchumi, kurahisisha usafiri wa wananchi na kuongeza ufanisi wa shughuli za biashara katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo yanayolizunguka.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi

slot gacor