[caption id="attachment_44225" align="aligncenter" width="773"] Mkuu wa Mkoawa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme akihutubia Kikao cha Baraza La Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma jana akiwa katika ziara ya kikazi ya Siku moja Wilayani Nyasa (Picha na Ofisi ya DED Nyasa)[/caption]
Na; Neto Credo - Nyasa
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Kwa kupata hati safi kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.
Akizungumza wakati akihutubia Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya hiyo lililofanyika jana katika Ukumbi wa Kepten John Komba uliopo mjini Mbamba-Bay ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Siku moja.
“Ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni matakwa ya Kikatiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kufanyiwa marekebisho ya mwaka 2005 kanuni Namba 10 ya Sheria ya Ukaguzi namba 11 ya mwaka 2008”. Alisisitiza Mhe. Mndeme
Aliongeza kuwa ukaguzi huo upo kisheria na ni haki ya Halmashuri kukaguliwa na isipokaguliwa ina haki ya kuhoji kwa nini hamjakaguliwa, kwani hoja zinawahusu wote yaani Madiwani nawatendaji kwa vile Halmashauri ina undwa na pande zote mbili.
Aidha alimpongeza Mhe. Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Martin Manyanya, Madiwani na Wataalam wote wa Wilaya ya Nyasa kwa kusimamia vema matumizi ya fedha za miradi na kupata Hati safi katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2017/2018, na kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2017/2018.
“Halmashauri hii imeshakaguliwa na CAG kwa miaka mitano kuanzia mwaka wa Fedha 2013/2014-2017/2018 katika kipindi hiki chote Halmashauri imepata Hati safi mara nne (4) na kupata hati yenye mashaka mara moja Hongereni sana kwa hati mnazoendelea kupata.haya ni matokeo ya utendaji kazi mzuri wenye mshikamano na ushirikiano.Inapotokea mmefanya vizuri hata sisi viongozi katika ngazi ya Mkoa tunafarijika sana kuona Halmashauri zetu zinafanya vizuri. Pia niwakumbushe pia msibweteke na kuona mmefika mwisho bali kwa mwaka unaofuata mzuie hoja sio kuzalisha hoja”, Alisisitiza Mhe. Mndeme.
Katika Hatua nyingine, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyasa Jimson Mhagama kwa kuteuliwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Nyasa na kumtaka ashirikiane na Madiwani, Wataalumu na Wananchi ili Wilaya iweze kuwa na Maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mh. Alto Komba alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kwa kufanya ziara ya siku moja Wilayani Nyasa na kuhudhuria Baraza la Madiwani na kusema kuwa wananyasa wamefarijika sana kwa ujio wake na wanamkaribisha siku nyingine akipata nafasi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme alifanya ziara ya siku moja wilayani hapa na kuhudhuria kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa na kukagua Miradi Mitatu ya Maendeleo .Miradi hiyo ni Jengo Ofisi na nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Jengo la Hosteli ya wasichana katika shule ya Sekondari Limbo na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa.