Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB) kwa kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara.
Mhandisi Gabriel, ametoa pongezi hizo wakati akifunga warsha ya siku mbili ya kujadili namna ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwenye miundombinu ya barabara na uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara,iliyofanyika jijini Mwanza.
Ambapo ameeleza kuwa, kupitia mfumo huo na kuwa na mikataba ya muda mrefu ya matengenezo ya kawaida ya barabara itasaidia sana kwani wamekuwa wakishuhudia mashimo hatarishi barabarani ambayo yamekuwa yakikaa muda mrefu bila kuzibwa kutokana na kukosekana taarifa kwa wakati na hivyo kusababisha ajali.
"Mfumo huu utatumiwa na wananchi kutoa taarifa za hali ya barabara na utawasaidia sana kwani awali walikuwa wanapata changamoto ya kutuma taarifa na wakati mwingine walikuwa wanawatumia watu ambao siyo sahihi na kufanya mchakato wa matengenezo kuchukua muda mrefu, hivyo naipongeza Bodi ya Mfuko wa Barabara kuunda mfumo huu ambao utasaidia kuboresha ubora wa miundombinu ya barabara nchini," ameeleza Mhandisi Gabriel.
Pia ametumia fursa hiyo kuwahimiza Wakala wa Barabara nchini kuandaa utaratibu endelevu wa kutumia taarifa kwa namna ambayo watakuwa wameshauriwa ikiwemo matumizi ya miongozo mbalimbali na taarifa ambayo imeandaliwa kwa ajili ya kuziwezesha nchi mbali mbali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye miundombinu ya barabara.
"Ni muhimu kuzihusisha taasisi na Wizara mbalimbali katika usanifu na kujenga miundombinu ya barabara, jambo hili ni muhimu kwani mbinu za kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwenye miundombinu ya barabara ni mtambuka na zinahitaji michango ya wadau mbalimbali," ameeleza Mhandisi Gabriel.
Kwa upande wake Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Eliud Nyauhenga, ameeleza kuwa wamezindua mfumo huo ili kuwashirikisha zaidi wananchi katika kufuatilia usalama na ubora wa miundombinu ya barabara.
Nyauhenga ameeleza kuwa wanafanya kazi kwa kutumia wataalamu wa ndani ya bodi ili kufuatilia kazi za barabara na katika kuongeza na kupanua wigo huo wameamua kutumia mfumo (app) ili kila mwananchi mwenye simu iwe kiswaswadu au simu janja (smart phone) aweze kushiriki katika kufuatilia hali ya barabara ikiwemo matengenezo ya barabara.
"Mwananchi akiona mahali matengenezo hayafanyiki sawa sawa anaweza kupiga picha, kuchukua video kidogo akatutumia na anapotutumia sisi taarifa moja kwa moja zinaenda kwa Meneja wa TARURA au TANROADS wa eneo husika, vile vile akiona shimo hatarishi anaweza pia kutuma taarifa ili TANROADS au TARURA wafanye matengenezo kwani ndio wajibu wao na sisi kazi yetu ni kusimamia matengenezo ya barabara yafanyike kwa wakati," ameeleza Nyauhenga.