Na; Mwandishi Wetu
Mradi wa GIRLS Inspire ulianzishwa kama sehemu ya kutekeleza mikakati ya kitaifa ya kuimarisha uwezo wa kuandaa na kutekeleza mipango ya kupiga vita ndoa za utotoni na kuwawezesha wanawake na wasichana walioathirika na ndoa za hizo kujikwamua kimaisha. Mradi huu unafadhiliwa serikali za Australia na Canada na kuratibiwa na kitengo cha elimu cha Jumuia ya Madola (Commonwealth of Learning COL).
Mradi unatekelezwa katika nchi tano ambazo ni Tanzania, Msumbiji, Pakistan, India na Bangladesh. Nchini Tanzania mradi huu umetekelezwa na Taasisi ya Elimu ya Watu wazima –TEWW kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la KIWOHEDE katika mikoa ya Rukwa, Dodoma na Lindi.
Kutokana na mafanikio yaliyopatikana, Tanzania imeteuliwa kuwa mwenyeji wa mkutana wa kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mradi huu utakaofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Mh. Ummy Mwalimu. Mkutano huu utawaleta pamoja wadau wote waliohusika katika utekelezaji wake pamoja na wabunge wa maeneo husika ili kujadili na kuona mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Katika utekelezaji wake nchini Tanzania, mradi huu uliwafikia wasichana na wanawake 3021 katika mikoa yote mitatu. .Mradi ulilenga wasichana na wanawake wenye umri kati miaka 10-24, ambao wameathiriwa na ndoa za utotoni au wako katika hatari ya kukumbwa na adha hiyo. Moja ya Lengo kuu la mradi huu ni kuwezesha wasichana na wanawake katika jamii zenye uhitaji kuwa na maisha bora na endelevu.
Kipekee, mradi huu ulilenga, kuongeza ushiriki wa wasichana na wanawake vijijini kwenye mipango bora ya kielimu kupitia ujifunzaji huria na masafa, Kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu bora na yenye kuzingatia mahitaji ya kijinsia kwa wasichana na wanawake walio vijijini kwa kutumia teknolojia na ujifunzaji huria na masafa Kuinua uwezo wa wasichana na wanawake wa vijijini kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kufanya maamuzi muhimu katika familia ikiwemo uzazi wa mpango.
Mradi huu ulilenga wilaya mbili kwa kila mkoa na kata moja kwa kila wilaya. TEWW ilijikita katika mikoa ya Rukwa na Dodoma katika wilaya za Kalambo, Nkasi, Bahi na Kongwa. Aidha, KIWOHEDE walilenga mkoa wa Lindi katika wilaya za Luangwa na Kilwa masoko.
Programu ya mafunzo ilihusisha maeneo matatu ya ujifunzaji ambayo ni: Stadi za maisha; zilihusisha masomo ya afya ya uzazi, malezi na makuzi ya watoto, elimu ya afya, elimu ya jinsia, elimu ya UKIMWI/VVU, elimu ya mazingira, elimu ya uraia na ujasiriamali
Taaluma; ilihusisha stadi za kuwasiliana kwa kutumia lugha ya kiswahili na English katika shughuli za kila siku, pia stadi za kutumia matendo ya hisabati katika maisha yao.
Ufundi wa awali; ulihusisha fani za kutengeneza sabuni za maji na mche, kutengeneza batiki na vikoi, kusindika vyakula kama unga wa lishe na siagi Utekelezaji wa mradi huu ulikuwa katika awamu mbili, ambapo walengwa walisajiliwa katika vituo vitatu vilivyoanzishwa katika kila kata. Vituo vingi vilianzishwa katika maeneo ya shule za msingi, vyuo vya maendeleo ya wananchi na kwenye ofisi za kata.