[caption id="attachment_40741" align="aligncenter" width="732"] Mratibu wa MKURABITA Bi. Seraphia Mgembe akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia hati za kimila za kumiliki ardhi kujiletea maendeleo wakati wa ufunguzi wa mafunzo yakuwajengea uwezo wakulima zaidi ya 100 wa Kijiji Cha Membe Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.[/caption]
Frank Mvungi
Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) umepongezwa kwa kuwawezesha wananchi Wilayani Chamwino mkoani Dodoma kwa kuwajengea uwezo ili waweze kutumia hati za kimila za kumiliki ardhi kujiletea maendeleo.
Akizungumza leo Wilayani humo wakati akifungua mafunzo kwa wakulima zaidi ya 100 wa Kijiji cha Membe mbunge wa jimbo hilo Mhe. Joel Mwaka amesema kuwa wananchi wanajengewa uwezo ili waweze kutumia hati hizo kujiletea maendeleo ikiwemo kuzitumia kama dhamana kuchukua mikopo katika Taasisi za fedha kama mabenki.
[caption id="attachment_40742" align="aligncenter" width="900"] Mbunge wa Jimbo la Chamwino Mhe. Joel Mwaka akifungua mafunzo kwa wakulima waliorasimisha mashamba yao na kupata hati za kimila za kumiliki ardhi kupitia Ofisi ya Rais, Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) leo Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.[/caption] “ Nawapongeza Ofisi ya Rais- MKURABITA kwa kuwezesha mashamba 1145 kupimwa na tayari hatimiliki za kimila 1000 zimeweza kuandaliwa ili kuwawezesha wananchi kuzitumia kujikwamua kiuchumi” Alisisitiza Mwaka.Akifafanua amesema kuwa kuna umuhimu wa kuunga mkono juhudi za MKURABITA kwani kati ya vijiji 107 vilivyopo katika halmashauri hiyo ni viwili tu vimebahatika kupata fursa ya kurasimishiwa ardhi na kujengewa uwezo kupitia mafunzo yanayoendeshwa na mpango huo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo.
[caption id="attachment_40743" align="aligncenter" width="900"] Mbunge wa Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma Mhe. Joel Mwaka akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya wananchi waliopatiwa hati za kimila za kumiliki ardhi baada ya kurasimisha mashamba yao katika Kijiji cha Membe.[/caption]Aliongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa wananchi kujitokeza kuchukua hati zao ili wazitumie kujikwanua kiuchumi kwa kuwa zimeshandaliwa na ziko tayari.
“ Faida za hati hizi ni pamoja na kuhakikisha usalama wa milki ya mkulima, kuongeza thamani ya ardhi na pia itasaidia kukuza uchumi wa Wilaya ya Chamwino na Taifa kwa ujumla” Alisisitiza Mwaka.
Alibainisha kuwa wakulima hao zaidi ya 100 watakuwa chachu ya kutosha kwa Wilaya hiyo na kuleta mabadiliko makubwa katika uzalishaji kwenye kilimo na ufugaji na hivyo kuongeza tija na kipato kwa wakulima wilayani humo.
Kwa upande wake Mratibu wa MKURABITA Bi. Seraphia Mgembe amesema kuwa Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa wanachi wanajikwamua kiuchumi kupitia uwezeshaji unaofanywa kwa kurasimisha mashamba ya wananchi na kuwapa hati ili waweze kuzitumia kujiletea maendeleo.
“ Mkitumia hati hizi vizuri kama Serikali ilivyodhamiria mtajikwamua kichumi kwani hapa kila aliyepewa tayari ajihesabu kuwa yeye ni mmiliki wa ardhi yenye thamani na inayoweza kuleta mageuzi makubwa katika maisha yake” Alisisitiza Bi. Mgembe.
Akifafanua zaidi amesema kuwa ni vyema wananchi wakaepuka vitendo vya kuuza ardhi zao kiholela badala yake wazitumie kwa tija hata pale wanapoamua kuuza sehemu ya maeneo yao walenge kujiletea maendeleo ili kuendana na dhana ya kujenga uchumi jumuishi inayosisistizwa na Serikali .
MKURABITA itaendesha mafunzo hayo kwa siku tatu yakilenga kuwajengea uwezo wakulima wa kijiji cha Membe kuzalisha kwa tija kupitia kilimo cha alizeti, ufugaji na pia watapata kujengewa uwezo kuhusu namna ya kutunza kumbukumbu, utafutaji fursa na namna ya kuzitumia, uandishi wa mpango wa biashara na uundaji wa vikundi vya hiari, utunzaji wa kumbukumbu na uthamini wa ardhi na utunzaji wa mazinsgira.