Veronica Simba – Singida
Serikali imemwagiza Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Pili (REA II) mkoani Singida, kuripoti polisi kila siku ili kuthibitisha kuwa yupo kazini hadi atakapokamilisha kazi hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Agosti 13, 2020 akiwa ziarani mkoani humo kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi husika, ambaye ni muunganiko wa Kampuni ya EMEC Engineering Ltd na Dynamic Engineering and System Company Ltd.
Alisema, mradi huo umekuwa ukisuasua tangu mwaka 2018 muda ambao ulipaswa kukamilika kutokana na sababu za kitaalamu na kiutendaji, hivyo Serikali imelazimika kuhakikisha unakamilika ifikapo Septemba 10, 2020.
Akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Waziri alimwelekeza Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Nchimbi kumsimamia Mkandarasi huyo na kutomruhusu kutoka nje ya mkoa huo hadi atakapokamilisha kazi. Aidha, alimwagiza kumweka chini ya ulinzi Mkandarasi endapo hatakamilisha kazi kwa wakati.
“Kuanzia kesho, viongozi na wataalamu wa Kampuni hii wawe wanaripoti polisi na kuweka saini ili kuthibitisha wapo kazini. Nami mniletee taarifa ya kila wiki ili nione nani alisaini na yupi hakusaini,” alisisitiza Waziri.
Alielekeza wasimamizi wa mradi huo kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufuatilia maendeleo ya kazi ya Mkandarasi huyo kwa muda wa siku saba na endapo hataonesha mwelekeo wa kuikamilisha kwa wakati, wafute Mkataba wake na wao wenyewe waikamilishe.
Sambamba na kufuta mkataba wake endapo hatakamilisha kazi, Waziri aliwaagiza TANESCO na REA kumchukulia Mkandarasi huyo hatua za kisheria na za kimkataba.
Waziri alimtaka Mkandarasi kuongeza idadi ya vibarua na aweke magenge manne katika kila Wilaya ili kuongeza kasi ya kazi.
Awali, wakiwasilisha kwa nyakati tofauti, taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Waziri, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi (REA), Mhandisi Jones Olotu na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida, Francis Kaggi, walikiri utendaji dhaifu wa Mkandarasi huyo.
Miongoni mwa changamoto walizozieleza ni pamoja na kasi isiyoridhisha ya Mkandarasi huyo kulingana na muda wake kimkataba. Aidha, walisema kuwa, Mkandarasi amesimika nguzo kwa muda mrefu pasipo kuvuta nyaya kwa baadhi ya vijiji.
Nyingine ni kuwa na magenge mawili tu na vibarua wachache wasioweza kukidhi nguvukazi inayohitajika ili kukamilisha kazi husika kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa, Dkt Nchimbi aliunga mkono kuwa utendaji wa Mkandarasi hauridhishi hivyo akamshukuru Waziri kwa kufuatilia na kuwekea mkazo utekelezaji wa Mradi husika.
Aliahidi kutekeleza yale yote yaliyoelekezwa na Waziri katika kuhakikisha Mkandarasi anafanya kazi yake ipasavyo.
Mkandarasi aliahidi mbele ya Waziri kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na kutekeleza maelekezo yake yote.
Mkandarasi huyo anatekeleza kazi katika Wilaya zote za Mkoa wa Singida ambapo mpaka sasa utekelezaji wake uko chini ya asilimia 20. Mradi unatakiwa uunganishie umeme wananchi 3,000 lakini hadi sasa waliounganishwa ni chini ya 1,000.
Katika hatua nyingine, Waziri amewaasa Watanzania waishio vijijini, ambao hawajafikiwa na umeme nchini kote kuwa wastahimilivu kwani Serikali itaanza kusambaza wakandarasi wa kufanya kazi hiyo kuanzia Agosti 20 hadi Septemba 20, mwaka huu.
Alisema Wakandarasi hao watafanya kazi ya kusambaza umeme kwa vijiji na vitongoji vyote vilivyosalia nchini ndani ya kipindi cha miezi 12.
Katika ziara hiyo, Waziri pia alikagua kazi inayoendelea ya kupeleka umeme katika kijiji cha Kisiriri, wilayani Iramba na kumtaka Mkandarasi kuwa amewasha umeme kabla ya Septemba 10, 2020.