Na. Thobias Robert.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augusto Lyatonga Mrema ameeleza kuwa mihimili mitatu ambayo ni Serikali, Bunge pamoja na Mahakama ipo huru katika utendaji kazi kinyume na inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati hapa nchini.
Mrema alieleza hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya shutuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa dhidi ya Serikali kuwa imekuwa ikiingilia mamlaka ya mihimili Bunge na Mahakama.
“Nimeamua kulisema hili kwa sababu kuna watu wanafikiri kuwa mihimili hii inatumiwa kinyume na katiba kwa madai haiwezi kutenda haki na kwamba Tanzania hakuna mgawanyiko wa madaraka jambo ambalo siyo la kweli,” alifafanua Mrema.
Aidha aliongeza kuwa, mihimili yote mitatu ina watendaji wake na inategemeana kwa mujibu wa katiba (check and balance). Pia amewaasa wananasiasa kuacha kuwapotosha na kuwachonganisha Wananchi na Serikali yao kwa kuwaaminisha kuwa hakuna uhuru wa mihimili hiyo.
“Mtu akisema kuwa mihimili hii haijitegemei na kwamba Rais ana mamlaka juu ya mihimili hiyo atakuwa anakosea kwani kila mhimili una watendaji wake hivyo makosa yanapojitokeza Rais hapaswi kulaumiwa, ndiyo maana nimeona niwaeleze Watanzania kwamba Rais haingilii mihimili hiyo,” ameongeza Mrema
Mrema alisisitiza uhuru wa mihimili hiyo kwa kutolea mfano wa kesi ya ‘kubambikiza’ dhidi yake aliyoshitakiwa na aliyekuwa Mkuu wa Polisi nchini IGP Omary Mahita juu ya kumkashifu Rais wa Awamu ya Tatu Benjamini Mkapa kupokea mgawo wa rushwa ya Sh. Milioni 900 kesi ambayo haikuwa kweli na aliachiwa huru na mhimili wa mahakama.
“Kesi hiyo Namba CR 2/1997 ya kubambikiziwa ilinidhoofisha sana kisiasa lakini naishukuru mahakama kwa kusimamia haki na kuniona sina hatia,” alisisitiza Mrema ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu.
Aidha Mrema aliwaomba watanzania wasidanganywe na wanasiasa juu ya mambo yanayotokea nchini kuhusu Rais na uendeshaji wa bunge.