Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mhe. Anastazia Wambura: "Sista Jean Pruitt Atakumbukwa kwa Mengi"
Sep 20, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_14575" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Anastazia Wambura akiongea na Viongozi mbalimbali pamoja na Watawa wa Shirika la Watawa wa MaryKnoll wakati wa Ibada ya kumuaga Marehemu Sista Jean Pruitt iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam. [/caption]

Na Benedict Liwenga-WHUSM.

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Anastazia Wambura amesema kwamba Mwanzilishi wa Nyumba ya Sanaa pamoja na Vituo mbalimbali vya Sanaa na Utamaduni nchini Tanzania, Marehemu Sista Jean Pruitt atakumbukwa kwa utu, upendo na kujituma wakati wote na kujitoa kwake kwa hali na mali katika kuviendeleza Vituo mbalimbali vya Sanaa na Utamaduni pamoja na kuendeleza maisha ya wenye mahitaji.

Mhe. Wambura ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Karimjee wakati wa Ibada ya kumuaga mtawa huyo aliyefariki dunia siku za hivi karibuni Jijini Arusha.

Amesema kwamba, mtawa huyo amekuwa akifanya kazi zake kwa bidii kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania na baadhi ya vituo ambavyo alivianzisha ni pamoja na Kituo cha Dogodogo Centre, TAMOFA, Vipaji, Alliance, huku akisaidia maendeleo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) katika kukuza vipaji vya vijana mbalimbali nchini.

[caption id="attachment_14579" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Anastazia Wambura akitoa heshima za mwisho mbele ya mwili wa marehemu Sista Jean Pruitt baada ya Ibada ya kumuaga mtawa huyo iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam. [/caption]

"Sista Jean atakumbukwa kwa jinsi alivyojitoa kusaidia na kuleta mabadiliko katika tasnia ya sanaa ikiwemo kutumia Nyumba ya Sanaa katika kuibua na kuviendeleza vipaji vya sanaa kwa Vijana wetu nchini", alisema Mhe. Wambura.

Aliongeza kuwa, mchango wake katika sanaa ulimwezesha mtawa huyo kupata tuzo mbalimbali zikiwemo, mwaka 1983 alipewa Tuzo Maalum na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo ilikua Tuzo ya Maisha pamoja na Tuzo ya Zeze iliyotolewa na uliokuwa Mfuko wa Utamaduni Tanzania.

  [caption id="attachment_14581" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba akitoa heshima za mwisho mbele ya mwili wa marehemu Sista Jean Pruitt baada ya Ibada ya kumuaga mtawa huyo iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam. [/caption]

Akisoma wasifu wa mtawa huyo, Mwakilishi wa Shirika la Masista wa Maryknoll, amesema kwamba, Sista Jean Pruitt alikuja Tanzania 1968 akifanya mambo mbalimbali kwa jamii ikiwemo masuala ya sanaa na watoto wadogo hususani wale wanaotoka katika mazingira magumu hivyo kazi zake alitekeleza kwa vitendo kuliko maneno.

"Sista Jean Pruitt alifanya shughuli mbalimbali ikiwemo miradi kwa vitendo zaidi, pia aliwalea watoto wengi zaidi nchini Tanzania kwa kuwasomesha na kuwasaidia vijana kuibua vipaji vyao", alisema Mwakilishi huyo.

Marehemu sista Jean Pruitt alizaliwa nchini Marekani Oktoba 17, 1939 katika Jimbo la Michigan na alijihusisha sana na masuala ya ustawi wa jamii akijikita katika masuala ya Sanaa na Watoto hususani nchini Tanzania pia ndiye mwanzilishi wa Nyumba ya Sanaa.

[caption id="attachment_14584" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya Masista toka Shirika la MaryKnoll pamoja na Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali wakifuatilia Ibada Maaalum ya kumuombea marehemu Sista Jean Pruitt iliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam. [/caption]

(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi