Kupitia uongozi mahiri na madhubuti wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko wa Utamaduni na Sanaa umefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi 5,250,070,500.89 kwa miradi 359 ya Sanaa iliyozalisha jumla ya ajira 497,213 ikiwemo miradi ya muziki 78, filamu 90, maonesho 65, ufundi 103 na lugha na fasihi 23.
Takwimu hizo zimetolewa leo Februari 28, 2025 jijini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Bi. Nyakaho Mahemba wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mfuko huo ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa Waandishi wa Habari ikiwa ni programu iliyoandaliwa na Idara hiyo.
Bi. Nyakaho ameitaja mikoa 18 iliyofikiwa na mikopo hiyo kuwa ni Dar- Es Salaam, Arusha, Morogoro, Pwani, Geita, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Kagera, Mara, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Simiyu, Kigoma na Katavi.
“Mfuko unatoa mikopo kwa kushirikiana na Benki ya CRDB na NBC ambapo lengo la ushirikiano huu ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kutumia utaalamu na uzoefu wao katika eneo la utoaji wa mikopo, usimamizi wa marejesho pamoja na ufuatiliaji wa miradi iliyowezeshwa”, amesema Bi. Nyakaho.
Aidha, kupitia uwezeshaji wa mikopo kisekta, sekta ya muziki imepata mikopo yenye thamani ya shilingi 1,246,215,189 kwa miradi 78, sekta ya filamu imepata mikopo yenye thamani ya shilingi 1,329,007,342.00 kwa miradi 90, sekta ya sanaa za ufundi imepata mikopo yenye thamani ya shilingi 1,550,060,050.00 kwa miradi 103 na sanaa za maonesho imepata mikopo ya shilingi 759,087,719.00 kwa miradi 65.
Katika upande wa uwezeshaji wa mikopo kimakundi, Bi. Nyakaho amesema kuwa Mfuko umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 5,250,070,501.89 iliyotolewa kwa miradi 359 ambapo shilingi 1,470,019,740 zilikopeshwa kwa makampuni 54, shilingi 525,007,050 zilikopeshwa kwa vikundi/Bendi 31, shilingi 1,312,517,625 zilikopeshwa kwa miradi 109 inayomilikiwa wanawake na shilingi 1,942,526,085. 89 kwa miradi 165 inayomilikiwa na wanaume.