Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Menejimenti ya Bot Yatakiwa Kushirikiana na Waandishi wa Habari
Dec 10, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Beatrice Lyimo

Naibu Gavana wa  Benki Kuu ya Tanzania  BoT (Uchumi na Sera) Dkt. Yamungu Kayandaliba ametoa wito kwa Menejimenti ya BoT kuhakikisha masuala ya Waandishi wa Habari yanashughulikiwa kwa haraka kwa lengo la habari kuweza kujulikana kwa wananchi.

Hayo yamesema na Mkurugenzi wa Tawi la BoT Dodoma Bw. Richard Wambali kwa niaba ya Dkt. Kayandabila wakati wa semina ya Waandishi wa Habari za uchumi na fedha leo jijini Dodoma.

"Kuchelewa kutoa majibu ya maswali au ufafanuzi wa matukio yanayohusu BoT ni kuwanyima wananchi haki yao ya msingi ya kujua Benki Kuu inafanya nini na kwanini inafanya hivyo" ameongeza Bw.Wambali.

Aidha, amesema kuwa katika kipindi cha miaka sita ambayo BoT imekuwa ikiendesha semina kama hii, imeshuhudia kuimarika kwa uandishi wa habari za Uchumi na Fedha katika vyombo mbalimbali vya habari.

Hivyo amewataka waandishi wa habari kuendelea kuzingatia maadili na kanuni zinazoongoza tasnia kwani wajibu wa wanahabari katika kuchangia maendeleo ustawi wa jamii ni mkubwa.

Mbali na hayo Dkt. Kayandaliba amewashukuru Waandishi wa Habari hapa nchini kwani mara kadhaa wamekuwa msaada katika kufikisha taarifa za BoT kwa umma na kwa wakati.

Akimuwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mkurugenzi Msaidizi wa Idara hiyo. Bi. Zamaradi Kawawa amewapongeza  BoT kwa kuandaa semina hiyo kwa Waandishi wa Habari kwani mafunzo hayo yanazidi kuwaongezea uwezo katika taaluma yao.

"Kwa sasa habari zinazohusu masuala ya Uchumi na Fedha zinaandikwa kwa ustadi na weledi wa hali ya juu kutokana na mafunzo haya mnayotoa kwao" ameongeza Bi. Zamaradi

Aidha, ametoa wito kwa Waandishi wa Habari kuiona semina hiyo kama fursa za kuelewa vyema namna ya kuandika taarifa za uchumi na fedha kwa maendeleo ya Taifa.

Nae Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki Bi. Zalia Mbeo amesema kuwa lengo la semina hiyo ni kuzidi kukuza uelewa kwenye uandishi wa habari za Uchumi na Fedha kwa waandishi hao na pia kuwajengea uwezo wa kuweza kusoma , kuzichambua na kuziandika taarifa na takwimu mbalimbali zinazotolewa na BOT.

Vilevile  kukuza mahusiano yaliyopo baina ya Benki Kuu ya Tanzania na tasnia ya habari nchini.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi