Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mchezaji wa Ujerumani Mwenye Asili ya Tanzania Kuutangaza Utalii Nje ya Nchi
Feb 21, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Grace Semfuko

Bodi  ya Utalii Tanzania (TTB) kwa kushirikiana na Magnet Youth Sports Organization ya Tanzania February 15 hadi 19 mwaka huu  walishirikiana  katika kuandaa safari ya kitalii ya kocha andreas Pach na Martin Hammel  wa Ujerumani ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio vya Utalii lengo likiwa ni kuutangaza Utalii wa Tanzania.

Andreas Pach na Mwenzake Martin Hammel ni Makocha ambao  wapo nchini Tanzania wakitokea kwenye mradi wa ITK Pathfinder 2019 uliopo chini ya Chuo Kikuu cha Leipzig cha nchini Ujerumani  mradi ambao unalenga kuwafundisha Makocha na Vijana kwenye mchezo wa Soka na kumtangaza Mchezaji nyota mwenye asili ya Tanzania anaechezea Ligi daraja la kwanza nchini Ujerumani Yusuph Poulsen.

Wakiwa Tanzania Makocha hao walipata nafasi ya kutoa mafunzo ya michezo kwa makocha 25 na Vijana 120 wa Kitanzania lengo likiwa ni kukuza Vipaji vya michezo  nchini.

Ujio wa makocha hao ni mwaliko wa Magnet Youth Sports Organization chini ya Mkurugenzi mwendeshaji wake Tuntufye Mwambusi  ambapo bodi ya utalii kupitia ujio huo wameamua kushirikiana katika kuutangaza utalii wa ndani ikiwemo Mlima Kilimanjaro

Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari Jijini Dar Es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alisema bodi hiyo imeanza mazungumzo ya awali na mchezaji huyo nyota Yusuph Poulsen ambaye anachezea ligi daraja la kwanza nchini Ujerumani ili kuutangaza Utalii wa ndani.

“kwetu sisi TTB tunachukulia ujio huu wa makocha hawa na mashirikiano yaliyopo kati ya ITK na Tanzania, na tumeanza mazungumzo na Mchezaji mwenye asili ya Tanzania Bw. Yusuph Poulsen ikiwa ni mkakati wetu wa kutumia watu maarufu katika kuutangaza utalii wa ndani na tunataka kumfanya kuwa  Balozi wa hiari wa utalii wa nchi yetu” alisema Jaji Mstaafu Thomas Mihayo.

Nae mmoja kati ya makocha hao wawili kutoka nchini Ujerumani Bw. Andreas Pach alisema Tanzania kuna Vipaji vingi vya michezo na hivyo ni muhimu kuviendeleza.

“tumefurahishwa kuona Watanzania ni watu wakarimu, Tanzania kuna vipaji vingi vya michezo na vipaji hivi vikiendelezwa tutakuwa mbali kimichezo, Poulsen anafanya vizuri sana kule Ujerumani” alisema Andreas Pach.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Magnet Youth Sports Organization Bw. Tuntufye Mwambusi alisema wataendelea kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania na wanamichezo katika kukuza Utalii wa Tanzania.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi