Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mchanga wa Dhahabu: Msimamo wa Magufuli Wailainisha Barrick
Jun 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

  • Habari za Taarifa za Kamati za Kuchunguza Makinia zatawala ulimwengu
  • Bosi wa Barrick akubali yaishe

Na Mwandishi Wetu.

Kwa kipindi cha zaidi miezi 4 sasa suala la mchanga wa dhahabu au Makinikia limetawala vichwa vya habari vya vyombo vya habari vya ndani na nje. Katika Makala hii Mwandishi Said Ameir wa Idara ya Habari- MAELEZO anaeleza uzito wa habari kwa kuangalia mustakbala wa makampuni ya madini na mataifa yanayotoka.

Ni dhahiri kuwa dunia hivi sasa inatafakari kuhusu namna ya kukabiliana na dharuba hii ya Rais Magufuli dhidi ya makampuni ya madini. Mabepari wa madini wamepatwa na kiwewe kwa sababu msimamo wa Rais Magufuli unawaamsha wengine waliolala nao kudai haki zao kama wanavyofanya watanzania.

Kwa lugha za vijana wa kileo wanasema ‘JPM ameliangusha ‘Dude’ ambalo limeleta taharuki kubwa katika viota vya biashara ya madini- mfano majiji ya London, New York, Geneva, Otawa, Vancouver na kwengineko katika sekta nzima ya biashara ya madini ulimwenguni.

Kwa karibu miezi miwili sasa vyombo vya habari katika majiji hayo vimekuwa vikiandika habari za Tanzania kuhusu mgogoro huo ambao umeitikisa sekta ya madini ulimwenguni.

Katika majarida ya sekta ya madini katika nchi za Canada, Australia, Marekani na Uingereza yamekuwa yakiandika habari za taarifa za Kamati za Rais kuchunguza mchanga wa madini. Kama kawaida mengi ya majarida hayo yanaelekeza shutuma kwa Mheshimiwa Rais na wengine kama si hivyo wamekuwa wakiripoti tu kile kinachotokea bila kutoa maoni.

Kwa wafuatiliaji wa masuala ya mwenendo wa uvunaji wa rasilimali katika nchi zinazoendelea unaofanywa na makampuni makubwa kutoka nchi tajiri hawatashangazwa hata kidogo na haya yanayotokea hivi sasa nchini Tanzania.

Kwa miaka mingi viongozi wa nchi masikini ikiwemo Tanzania wamekuwa wakipiga kelele dhidi ya makampuni hayo kuvuna maliasili za nchi zao kwa kutumia mikataba ya kinyonyaji ambayo pamoja na mambo mengine ni matokeo ya udhaifu wa nchi masikini wa kukosa utaalamu na uzoefu katika sekta hiyo.

Katika nchi tajiri, mara nyingi tumeona katika mikutano ya kimataifa, sauti za kupinga vitendo hivyo zimekuwa zikipazwa na wanaharakati wanaotetea rasilimali za nchi masikini na wale wa haki za binadamu pekee huku viongozi wa nchi hizo wakilipuuzia suala hilo kwa manufaa ya makampuni yao.

Si katika mikutano hiyo wala wakiwa nchini mwao, hatujaona viongozi wa nchi tajiri wakichukua hatua madhubuti kuyadhibiti makampuni yao kuacha kuzinyonya nchi masikini kupitia mikataba ya uvunaji wa maliasili. Kama ilivyoelezwa jukumu hilo la kupinga uporaji wa rasilimali za nchi masikini limeachwa kwa waharakati pekee.

Wamekuwa wakizitia nchi masikini katika migogoro huku wakivuna maliasili za nchi hizo wakati huo huo kwa kutumia wasomi na wataalamu wao kuendeleza ukoloni mamboleo wa kifikra na kuleta nadharia mpya kama “laana ya maliasili” (natural resource curse) kuonesha kuwa kosa ni la nchi masikini si lao. Kwamba maliasili zimeleta laana… tunapigana na kuuana na kumbe nyuma wao ndio chanzo.

Kama inavyojitokeza hapa nyumbani, huko ‘duniani’ nako wako wanaowatetea wanyonyaji kama Acacia na wala haishangazi kwa kuwa wana maslahi yao lakini pia wako wanaowatetea watanzania kwa sababu ni waumini wa kukataa unyonyaji hata kama unafanywa na ndugu zao.

Nchini Canada kwenyewe, mshikemshike umewakuta viongozi wa Kampuni ya Barrick inayomiliki asilimia kubwa ya hisa za kampuni ya Acacia kwani wanaharakati wameanza kuhoji usafi wa uongozi wa kampuni hiyo kwamba wanawezaje kuendeleza unyonyaji na udanganyifu kwa  nchi masikini.

Ieleweke kuwa Acacia wameikosesha Serikali mapato yake kwa njia za udanganyifu kitendo ambacho kinaonesha kampuni hiyo haina maadili na si adilifu; inakwenda kinyume na misingi ya haki na utawala bora.

Kwa bahati mbaya huko ‘duniani’ na hata hapa Tanzania wanaowatetea Acacia wanazungumzia zaidi zuio la Rais la kusafirisha mchanga nchi za nje na hawaoni kabisa ubaya wa vitendo hivi vya udanganyifu kana kwamba wamevaa miwazi za mbao. Hawazunguzii kabisa hasara ya zaidi ya shilingi trilioni 108 iliyopata Tanzania na wananchi wake.

Hawataki kuona kuwa vitendo hivyo ni vya kuhujumu uchumi; wanakwepa kodi za aina mbalimbali kwa kutoeleza hali halisi ya biashara yao kwa njia mbalimbali kama kuwasilisha nyaraka zisizo kamilifu kwa kupunguza idadi ya makontena, kutotoa taarifa za madini mengine yanayopatikana katika mchanga unaosafirishwa.

Katika nchi za Magharibi makosa haya hayavumiliwi na ni kati ya makossa makubwa yenye adhabu kali, na katika baadhi ya nchi, kuliko za kosa la kuua kwa kukusudia. Kwa hiyo inapotokea huku kwetu, baadhi wakayaona madogo inashangaza!

Ni ukweli usiopingika kuwa ‘kishindo’ cha Rais Magufuli sio tu kimetikisa hisa za Kampuni ya Acacia katika masoko ya hisa ya London na New York lakini pia imetia doa katika taswira nzima ya kampuni hiyo na Kampuni mama ya Barrick.

Ukitaka kupima uzito wa jambo hili ni kuangalia namna ya hatua ilizozichukua kampuni ya Barrick kuja Tanzania kuonana na Rais Magufuli. Ujio wa Profesa John Thornton ambaye ni Mwenyekiti wa Barrick usichukuliwe kuwa ni kitendo cha kawaida bali ni hatua muhimu kwa kampuni kutafuta suluhu kwa njia za amani.

Wahenga walisema’kweli ikidhihiri uongo hujitenga’ na ndivyo ilivyo kwani Barrick walishatanabahi kuwa taarifa zote mbili zina ukweli na Rais Magufuli asingeweza kusema hicho alichokisema dhidi ya Acacia kama hana hakika ya anachokisema.

Tofauti na baadhi ya watu wanavyofikiri, Barrick na Acacia haimuoni Rais Magufuli kama mtu pekee bali wanaangalia pia uwezo na ushawishi iliyonayo Tanzania katika ngazi ya kidiplomasia. Wamepima taswira ya Rais Magufuli hivi sasa kwa kuzingatia namna anavyoonekana shujaa nje ya Tanzania. Katika hali hiyo Barrick na Acacia wamejiona hawana budi waepuke kiburi badala yake watafute njia salama na itakayowapunguzia machungu ya kuzidi kuchafua jina la kampuni yao.

Profesa Thornton, alisindikizwa na Balozi wa Canada nchini Bwana Ian Myles wakati alipokutana na Rais Magufuli. Hili linathibitisha uzito zaidi wa tuhuma dhidi ya Acacia. Kwa wafuatiliaji wa masuala ya kidiplomasia watakubaliana na mwandishi wa makala haya kuwa kadhia hii imeifedhehesha Serikali ya Canada na ndio maana balozi alihudhuria mazungumzo hayo.

Kama inavyojulikana Canada ni miongoni mwa ‘vinara’ wa kuhubiri na kufundisha utawala bora kwa nchi zetu na katika kufaya hivyo nchi hizi zinatuaminisha kuwa nchi zao na taasisi zao zinaendeshwa kwa misingi ya uwazi, sheria na utawala bora.

Inapotokea hali kama hii kampuni yao kushutumiwa kwa mambo ambayo wao wenyewe wanayapinga na wakati mwingine kuwadhihaki hata viongozi wa mataifa masikini nao uso ‘unawashuka’. Ni fedheha kubwa kwao!

Akiwa mwanadiplomasia namba moja wa Tanzania, Rais Magufuli amekuwa muwazi kwa yeyote kama ambavyo ‘hapepesi macho’ kwa wananchi wake katika kusema ukweli ndivyo hivo kwa wageni.

Kwa hivyo hapana shaka yeyote, kuwa Rais Magufuli aliwaeleza wageni wake kila kitu kinagaubaga na kwa hisia zile zile ambazo alizionesha kwa watanzania wakati akipokea taarifa za Kamati alizoziunda.

Ndio maana Profesa Thornton alizielewa vyema hoja za Rais Magufuli na kuzipima uzito wake unaostahiki ndipo alitafakari na kutoa ombi la kutaka majadiliano na Serikali na hapo hapo aliahidi kurejesha fedha zote ambazo Tanzania ilipaswa kupata katika biashara ya madini ya Kampuni ya Acacia.

Kuja kwa ‘matawi ya chini’ kwa Mkuu huyo wa Barrick kunaonesha pia uwezo wa kampuni ya Barrick kupima athari za kulipeleka jambo hili katika vyombo vya usuluhisho wa kimataifa kwa kampuni yake.

Ni mtu mwenye matatizo ya kufikiri tu anayeweza kudhani katika ‘timbwili’ hili Acacia na Barrick wako salama salimini. Kesi hii ikifika katika mahakama za kimataifa itakuwa ni kashfa nzito kwa Acacia na wanahisa wake na inaweza kuharibu kabisa biashara zao.

Itakuwa hivyo kwa misingi kuwa ushahidi utakaotolewa ‘utaivua nguo’ kampuni hiyo na inaweza ukawa mwanzo wa kuporomoka biashara yake. Kwa kutanabahi huko ndiko kulikomfanya Profesa Thornton akasema ‘funika kombe mwanaharamu apite’.Tuyazungumze!

Aidha kesi hiyo inaweza kuchochea migogoro mingine sio dhidi ya kampuni hiyo tu lakini dhidi ya makampuni mengine ya madini kama si ya hata mafuta na gesi katika nchi kama zetu ambazo zinanyonywa na makampuni hayo kupitia mbinu chafu kama zinazotumika humu nchini.

Kwa hiyo, kama walivyosema wahenga ‘heri nusu ya shari kuliko shari kamili’ ndio tafsiri ya hatua ya Kiongozi wa Barrick Profesa Thornton ya kutaka suluhu kwa mazungumzo na kwa hakika kwa lugha nyingine ni sawa na kusema ‘amekubali yaishe’.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi