Na Shamimu Nyaki –WHUSM, Lindi.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kwamba Serikali haijazuia maudhui ya redio za nje kusikia nchini bali imeagiza maudhui hayo yapate kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ndio inayosimamia maudhui ya utangazaji nchini.
Waziri Mwakyembe ameyasema hayo katika mahojiano na redio Mashujaa FM ya mkoani Lindi ambapo amesema kwamba redio za nje zinapaswa kuitaarifu TCRA maudhui inayotaka kurusha, lengo likiwa ni kulinda na kuheshimu maadili ya nchi.
“Serikali haijakataza redio za ndani kujiunga au kupokea maudhui kutoka redio na televisheni za nje bali kinachotakiwa kufanyika ni kufuata utaratibu ambao Serikali imeweka, nchi yetu sio ya kupokea na kutoa kila kitu tayari ni nchi huru hivyo lazima iheshimiwe”, alisema Dkt.Mwakyembe.
Katika hatua nyingine Waziri Mwakyembe ametumia nafasi hiyo kueleza mafanikio ya sekta anazozisimamia ambapo amesema kuwa sekta ya habari imeendelea kufanya mageuzi makubwa ikiwa ni pamoja na kusimamia Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambapo amewataka wanahabari kufanya kazi kwa kuzingatia sheria hiyo ambayo imeeleza kwa kina suala la weledi katika taaluma, ukweli na uwazi katika kuchakata habari.
Mhe. Waziri ameongeza kuwa Sekta ya Michezo imepata mafanikio mengi ikiwemo nchi kushiriki AFCON baada ya takriban miaka 30, timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Kilimanjaro Queens na Twiga stars kutwaa ubingwa wa CECAFA na COSAFA kwa vipindi tofauti.
Sekta hiyo pia imefanikiwa kurudisha hadhi ya mchezo wa ngumi ambapo tangu ilipotungwa Sheria ya kusimamia mchezo huo mwaka 2018 mafanikio mengi yameonekana kwa wanamasubwi ikiwemo kutwaa mikanda takriban 9 ya uzito mbalimbali na idadi ya wanamasubwi imeongezeka.
Akizungumzia mchakato wa kubadilisha jina la Uwanja wa Taifa kuitwa Benjamin Mkapa Stadium amesema nyaraka mbalimbali zimekamilika kwa ajili ya jina hilo,huku akiongeza kuwa uwanja huo ni ahadi aliyotoa mhe Rais wa Awamu ya Tatu, Marehemu Benjamin Mkapa katika kipindi cha awamu ya pili cha uongozi wake ambayo aliitimiza na imechangia mafanikio makubwa katika sekta ya michezo.
“Uwanja wa Dodoma nao mchakato wake umefikia pazuri ikiwemo kukamilika kwa michoro na tathmini nyingine na hivyo kazi itaanza mara moja na ukikamilika uwanja huo utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji takriban elfu 80” aliongeza, Mhe.Mwakyembe.
Hata hivyo, Dkt.Mwakymbe ameliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuanisha vigezo vinavyotakiwa kwa mchezaji wa nje hapa nchini ikiwemo mchezaji huyo kuwa na sifa ya kucheza timu ya Taifa analotaka,awe anacheza ligi kuu, na iwapo anatoka nchi ambayo iko ndani ya hamsini bora katika orodha ya FIFA basi awe anacheza angalau ligi daraja la kwanza.
Aidha Dkt.Mwakyembe amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja ambao Tanzania imekuwa Mwenyekiti wa Nchi za Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),imefanikiwa kushawishi nchi za jumuiya hiyo kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ndani ya jumuiya hiyo,hatua ambayo imesaidia kukuza na kuendeleza lugha hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo fursa za kufundisha kiswahili ndani ya jumuiya pamoja na nchi nyingine.
Mhe.Mwakyembe amewataka waandishi wa habari katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika kampeni na hatimaye Uchaguzi Mkuu,lazima watumie kalamu zao vizuri kwa kuandika na kutangaza habari zenye ukweli,uwazi,zilizochakatwa vizuri,ambazo hazionyeshi upendeleo wowote kama ambavyo taaluma ya habari inataka.