Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mapori ya Akiba kuwa hifadhi za Taifa
Feb 09, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_40304" align="aligncenter" width="900"] Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamis Kigwangala akijibu hoja za wabunge wakati akihitimisha hoja ya azimio la Bunge kupandisha hadhi mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika –Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa leo Bungeni Jijini Dodoma.[/caption]

Na, Adelina Johnbosco, MAELEZO, Dodoma.

Wabunge wameridhia kupandisha hadhi mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda, na Rumanyika – Orugundu kuwa hifadhi za Taifa ambayo yatakuwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA)

Maridhiano hayo yamefikiwa kwenye mkutano wa kumi na nne wa bunge la kumi na moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe Februari 9, 2019.

Katika upandishwaji hadhi wa mapori hayo, mapori matatu ya Biharamulo, Burigi na Kimisi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,702 yameunganishwa kwa pamoja ili kuleta ufanisi wa uzalishaji wake, mapori haya yanazungukwa na kata 18 zenye vijiji 48 zikihusishwa wilaya za Biharamulo,Ngara, Karagwe na Muleba mkoani Kagera na wilaya ya Chato mkoani Geita.

Aidha mapori ya akiba ya Ibanda na Rumanyika – Orugundu yanazungukwa na kata 12 zenye vijiji 24 katika kata ya Kyerwa.

Akisoma azimio hilo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema sera ya wanyamapori ni kudumisha uhifadhi endelevu kwa kuanzisha na kuboresha maeneo yaliyohifadhiwa kwa madhumuni ya kulinda baioanuwai katika hifadhi za Taifa, Mapori ya akiba, Mapori Tengefu, na maeneo ya wazi.

Mchakato wa kisheria wa kupandisha hadhi mapori ya akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa hifadhi za taifa umekamilika na mipaka yake tayari imebainishwa,

Hatua hiyo pia itahusisha zoezi la kuhamisha wanyama, kuwatafuta na kuwarudisha wanyama wote waliotoroka ama kuhama kutoka hifadhi hizo ili warudi na kuendelea kuwa vivutio katika maeneo yao husika katika hifadhi.

Imeelezwa kwamba, mapori ya Ibanda yalianzishwa yakiwa na kilometa za mraba 1000, mwaka 2000 ukubwa wake ulipungua hadi kilometa za mraba 549 kutokana na kutokuwepo alama za mipaka iliyopelekea kuvamiwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo makazi, kilimo na ufugaji.

Akisisitiza juu ya azimio la kupandishwa hadhi mapori hayo, Naibu Waziri wa Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula, amesema kuwa uamuzi huu utakuwa ni ufumbuzi wa changamoto hizo zilizopelekea maeneo hayo muhimu kuwa na mchango mdogo kiuchumi.

Akibainisha sababu za kuu za kupandishwa hadhi mapori hayo, Waziri Kigwangalla amesema ni pamoja na wageni wengi kutembelea kutokana na uwepo wa wanyamapori adimu kama vile nzohe, palahala, chui, korongo, taya, nyangumi, na miti aina ya misambya, pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwemo Ziwa Burigi, Nyamalebe, Ngoma na Kasinga ikiwemo utunzaji wa mazalia ya samaki, uwindaji wa kitalii na utunzaji wa maji moto.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi