UTANGULIZI
- Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha wabunge wote kukutana tena hapa Jijini Dodoma, kupokea mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, kwa mujibu wa Kanuni ya 97 fasili ya (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016. Aidha, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu umoja na amani.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki (Mb), Mheshimiwa Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb), Mheshimiwa Prof. Palamagamba Aidan Kabudi (Mb), Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko (Mb), Mheshimiwa Joseph George Kakunda (Mb) na Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga (Mb) kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mawaziri ili kuongoza wizara mbalimbali. Ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Mawaziri mlioteuliwa na Waheshimiwa Wabunge wote mtaendelea kunipatia ushirikiano katika kuijenga nchi yetu kwa manufaa ya Watanzania wote.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii inawasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2019/20 ambayo imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza ni tathmini ya mwenendo wa hali ya uchumi. Sehemu ya pili ni Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/19 na Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/20. Sehemu ya tatu ni tathmini ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2018/19 na mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20.
SEHEMU YA KWANZA
TATHMINI YA MWENENDO WA HALI UCHUMI
- Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuiandaa nchi kuelekea uchumi wa kipato cha kati, uchumi umeendelea kuimarika. Pato la Taifa kwa kutumia mwaka wa kizio 2015 linaonesha kuwa katika robo ya tatu (Julai hadi Septemba) ya mwaka 2018, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.8 ikilinganishwa na asilimia 5.0 kipindi kama hicho mwaka 2017. Shughuli za kiuchumi zilizokuwa kwa kasi kubwa ya ukuaji ni afya (asilimia 13.2), usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 12.4); Maji (asilimia 10.7); Ujenzi (asilimia 7.4); Habari na Mawasiliano (asilimia 7.3); viwanda (asilimia 7.3); na Biashara na Matengenezo (asilimia 7.3).
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018, mwenendo wa mfumuko wa bei nchini uliendelea kuwa tulivu katika wigo wa tarakimu moja kutokana na kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini na nchi jirani pamoja na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti za Serikali. Mfumuko wa bei ulipungua kutoka wastani wa asilimia 4.0 Januari 2018, hadi kufikia asilimia 3.4 Juni 2018 na kuendelea kupungua zaidi hadi asilimia 3.0 Januari 2019.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka unaoishia Januari 2019 thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nchi za nje ilikuwa dola za Marekani milioni 8,300.0 na thamani ya bidhaa na huduma zilizonunuliwa kutoka nje ilikuwa dola za Marekani milioni 10,462.6. Kwa upande wa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje ilikuwa dola za Marekani milioni 2,982.2 kutokana na kuongezeka kwa thamani ya bidhaa za mitaji zilizoagizwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya miradi mikubwa ya maendeleo. Kwa matokeo hayo akiba ya fedha za kigeni ni Dola za Marekani milioni 4,884.4 Januari 2019, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha takribani miezi 4.8. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi 4.5.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.6 katika mwaka 2018 ikilinganishwa na ongezeko la wastani wa asilimia 5.5 katika kipindi cha mwaka 2017. Mwenendo huo ulichangiwa na kuimarika kwa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kulikotokana na jitihada za Serikali kupitia Benki Kuu katika kuchochea ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi. Riba za dhamana za muda mfupi za Serikali zilipungua hadi wastani wa asilimia 6.4 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 11.1 mwaka 2017. Vile vile, riba za mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi zimeendelea kupungua kutoka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2017 hadi wastani wa asilimia 17.4 mwaka 2018.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kuimarika kufuatia utekelezaji wa sera ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi pamoja na jitihada zilizochukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu katika kuchochea ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi. Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka ambapo Januari 2019 ilikuwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 2.1 Januari 2018. Sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuelekezwa katika shughuli binafsi (asilimia 27.9 ya mikopo yote) ikifuatiwa na shughuli za biashara zilizopata asilimia 18.4, uzalishaji viwandani (asilimia 11.6) na kilimo (asilimia 7.8).
- Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo wa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani umeendelea kuwa tulivu ambapo katika mwaka 2018, Dola moja ya Marekani ilinunuliwa kwa wastani wa Shilingi 2,263.8. Hii ni kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha, usimamizi thabiti wa mapato na matumizi ya Serikali, matumizi ya gesi asilia na umeme wa maji badala ya mafuta katika kuzalisha umeme na baadhi ya viwanda nchini kuzalisha bidhaa ambazo awali zilikua zikiagizwa kwa wingi kutoka nje.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano, itaendelea kutekeleza sera madhubuti za fedha na bajeti ili kuhakikisha uchumi wa nchi yetu unaendelea kuimarika.
SEHEMU YA PILI
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2018/19 NA MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2019/20
- TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2018/19
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/19, Serikali ilitenga Shilingi bilioni 12,007.3 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, zikijumuisha Shilingi bilioni 9,876.4 fedha za ndani na Shilingi bilioni 2,130.9 fedha za nje. Hadi Januari 2019, jumla ya Shilingi bilioni 2,788.5 zilitolewa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, Shilingi bilioni 144 zilipokelewa kutoka kwa Washirika wa Maendeleo na kupelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretaieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Vile vile, Shilingi bilioni 3,803.4 zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Serikali imeshatenga na inatarajia kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 1,433.8 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo mradi wa kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji Mto Rufiji (MW 2,115).
- Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo katika mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:
(i) Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge: Ujenzi wa kipande cha
Dar es Salaam – Morogoro (km 300) unaendelea vizuri kama ilivyopangwa, ambapo shughuli zinazoendelea ni ujenzi wa madaraja, makalavati, daraja lenye urefu wa km 2.54 katikati ya jiji la Dar es Salaam, ukataji wa miinuko, ujazaji wa mabonde na utandikaji wa reli. Katika kipande cha
Morogoro – Makutupora (km 422), kazi zinazoendelea ni pamoja na ukataji wa miinuko na ujazaji wa mabonde, usanifu wa njia na ujenzi wa kambi za Kilosa na Ihumwa. Kwa upande wa kipande cha
Isaka – Rusumo (km 371), hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa njia ya reli. Aidha, taratibu za ununuzi wa mabehewa, injini na mitambo itakayotumika kutoa huduma ya usafiri kwenye reli ya
Standard Gauge zipo katika hatua za mwisho.
Katika miradi inayogharamiwa na mfuko wa reli, shughuli zilizofanyika ni: kununua vichwa 11 vya treni kwa ajili reli ya kati; kuendelea na ukarabati wa reli ya Tanga - Arusha (km 439) ambapo kipande cha Tanga – Mombo (km 129) kimeanza kufanya kazi ya kusafirisha mizigo na ukarabati wa vipande vya Mombo – Same (km124) na Same – Arusha (km 186) unaendelea. Aidha, kazi ya ukarabati wa mabehewa inaendelea ambapo hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa ukarabati wa mabehewa 15.
(ii) Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Rufiji - MW 2,115: Hatua iliyofikiwa ni: kupatikana kwa mkandarasi wa mradi wa kufua umeme utokanao na nguvu ya maji katika Mto Rufiji ambaye ni Kampuni ya Ubia kati ya
Arab Contractors na
Elsewedy Electric S.A.E kutoka Misri ambapo mkataba wa ujenzi umesainiwa na mkandarasi alikabidhiwa eneo la mradi mwezi Februari 2019. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu wezeshi ikijumuisha njia ya umeme wa msongo wa kV 33 kutoka Msamvu hadi eneo la mradi; mifumo ya huduma ya maji na ya mawasiliano ya simu; kukamilika kwa ujenzi wa nyumba 10 na kuendelea na ukarabati wa nyumba 28 za iliyokuwa kambi ya RUBADA; ujenzi wa barabara za Kibiti - Mloka – Mtemere – Matambwe
Junction – Mto Rufiji (km 210) na Ubena Zomozi – Mvuha – Kisaki – Mtemere
Junction (km 178.39) zimekamilika.
(iii) Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Hatua iliyofikiwa ni: kuwasili kwa ndege nyingine tatu, moja ikiwa ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na mbili zikiwa ni Airbus A220-300, na hivyo kufanya idadi ya ndege zilizonunuliwa kuwa sita; kulipa sehemu ya gharama za ununuzi wa ndege moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na Bombadier Q400 zinazotarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwaka 2019. Kufuatia hatua hiyo, ATCL itaanzisha safari za ndege kwenda nchini China na India ambazo kimkakati ndizo masoko mapya ya utalii.
(iv) Miradi ya Umeme: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa km 250 ya msongo wa kV 220
Makambako – Songea pamoja na vituo vitatu vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea, hivyo kuwezesha mikoa ya Njombe na Ruvuma kuunganishwa katika Gridi ya Taifa; kuendelea na mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 wa Singida – Arusha – Namanga wenye urefu wa km 414; kuendelea na miradi ya kusafirisha umeme ya Geita – Nyakanazi (kV 220), Rusumo – Nyakanazi (kV 220) na Bulyankulu – Geita (kV 220); kuendelea na utekelezaji wa mradi wa
Kusambaza Umeme Vijijini na Makao Makuu ya Wilaya ambapo vijiji 1,782 na wateja 96,832 wameunganishiwa umeme hivyo kufikia jumla ya vijiji 1,039 vilivyounganishwa na umeme; kukamilisha utengenezaji wa mitambo minne ya kufua umeme na kupelekwa mitambo miwili ya kufua umeme katika eneo la mradi wa
Kinyerezi I Extension – MW 185; Mradi wa Kufua Umeme wa
Rusumo MW 80: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa barabara za kuingia eneo la mradi; kukamilika kwa ujenzi wa kikinga maji; kuanza kazi ya kuchimba handaki la kupitisha maji; kuendelea na uchimbaji wa eneo itakapofungwa mitambo; na kukamilika kwa ujenzi wa nyumba mbili kati ya tano za wafanyakazi.
(v) Huduma za Maji Mijini na Vijijini: miradi 65 imekamilika na kufanya jumla ya miradi yote iliyokamilika kufikia 1,659 na vituo vya kuchotea maji kuongezeka hadi 131,370 na kuhudumia wananchi 25,359,290. Upatikanaji wa huduma za maji Jijini Dar es Salaam umefikia asilimia 85, katika mikoa mingine asilimia 80, miji midogo asilimia 64 na vijijini asilimia 64.8. Aidha, utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mengine unaendelea katika hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa maji wa Ziwa Victoria – Igunga - Nzega na Tabora, mradi wa maji katika jiji la Arusha na Same – Mwanga - Korogwe. Vile vile, utekelezaji wa mradi wa maji katika miji 28 wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 465 upo katika hatua za kumpata Mtaalamu Mwelekezi na Mkandarasi wa mradi.
(vi) Miradi ya Afya: Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa asilimia 96. Hatua nyingine zilizofikiwa ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa jengo la vifaa vya uchunguzi (X–Ray Building) na kununua vifaa vya tiba ya mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya; na kuongeza utoaji wa chanjo kufikia asilimia 97. Aidha, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya afya katika ngazi zote ikijumuisha ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa, kanda na kitaifa; ujenzi wa hospitali za halmashauri 67; ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya 352; kuajiriwa kwa watumishi wa sekta ya afya 7,680; ujenzi wa nyumba 310 za watumishi wa afya; ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za halmashauri, Vituo vya Afya na Zahanati. Serikali imeendelea kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na hivyo kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi katika hospitali za Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Taasisi ya Mifupa (MOI), hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi – Mloganzila.
(vii) Miradi ya Elimu: Serikali imeendelea kugharamia elimumsingi bila ada ambapo kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 24.4 kinatumika. Hatua nyingine zilizofikiwa ni: ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikijumuisha madarasa 870, matundu ya vyoo 1,958, mabweni 210, mabwalo 79; ukarabati wa shule kongwe; ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vya ualimu Ndala, Shinyanga, Patandi, Mpuguso na Murutunguru; kukamilisha maboma ya madarasa, mabweni na nyumba za walimu 39; ukarabati wa vyuo vya kati 20 kati ya 54 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs), nyumba za walimu 39; kukamilika na kuzinduliwa kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; ujenzi wa mabweni katika Chuo Kikuu cha Mzumbe yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000; ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vikuu vya Sokoine na Dar es Saaalm; na mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu 119,214; uimarishaji wa vyuo 10 vipya vya VETA na kukuza ujuzi kwa vijana; na ujenzi wa shule kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika chuo cha Ualimu Patandi.
(viii) Kilimo: Utoshelevu wa Chakula kwa mwaka 2018/19 umefikia asilimia 124. Aidha, Serikali imeanza utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) na mkazo umewekwa katika kuendeleza mazao ya kimkakati yakiwemo Kahawa, Pamba, Chai, Korosho, Tumbaku, Alizeti, Michikichi, Mpunga na Mahindi. Ili kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo, Serikali inaendelea kuimarisha shughuli za ushirika, ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 250,000 katika kanda saba, kuongeza uzalishaji wa mbegu za mafuta hususan alizeti na michikichi, kuimarisha shughuli za utafiti wa mazao, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kwa kufufua vinu vya kusindika mazao ya nafaka na mafuta, kudhibiti visumbufu vya mazao, kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kuimarisha mifumo ya masoko ya mazao. Vile vile, Serikali imeanza kuboresha mifumo ya takwimu za kilimo kwa kuanza usajili wa Wakulima.
(ix) Mifugo: Hatua iliyofikiwa ni kuendelea kuimarisha vituo 3 vya kuzalisha vifaranga vya samaki vya Kingolwira (Morogoro), Mwampuli (Igunga) na Ruhila (Songea) kwa kuzalisha na kusambaza vifaranga vya samaki kwa wafugaji wa samaki wakiwemo vijana. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na sekta Binafsi imeweza kuzalisha jumla ya vifaranga 17,301,076 kama ifuatavyo: kambamiti 11,080,000, sato 5,072,800 na kambale 1,148,276. Vile vile, jumla ya wananchi 6,995 wamepatiwa elimu ya ugani katika ukuzaji wa viumbe maji.
(x) Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania): Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa tathmini ya athari za mazingira na jamii kwa upande wa Tanzania; kukamilika kwa tafiti za kijiolojia katika eneo la Chongoleani; kukamilika kwa tathmini za Kijiolojia na Kijiofizikia katika eneo la mkuza wa bomba; na kutwaa ardhi eneo la Bandari – Tanga (Chongoleani) kutakapojengwa miundombinu ya kuhifadhi mafuta.
(xi) Miradi ya Viwanda: Kiwanda cha Kuunganisha Matrekta (TAMCO, Kibaha): Hatua iliyofikiwa ni: kuingiza matrekta 822 aina ya URSUS (semi knocked down) ambapo matrekta 571 yameunganishwa na matrekta 339 yameuzwa;
Kituo cha Zana za Kilimo na Ufundi Vijijini – CAMARTEC: kutengeneza zana zikijumuisha mashine 64 za kupandia mbegu za pamba, kusaga karanga, kukausha mbogamboga na kukata majani pamoja na ujenzi wa mitambo 55 ya
biogas;
SIDO: kuendelea na ujenzi wa majengo ya viwanda 11 katika Mikoa ya Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Manyara, Mtwara na Simiyu na ujenzi wa ofisi za SIDO katika mikoa mipya ya Geita na Katavi.
(xii) Miundombinu ya Biashara ya Madini: Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kuboresha mazingira ya biashara kwenye sekta ya madini ikihusisha: vituo vya umahiri katika mikoa saba, vituo vitatu vya mfano, jengo la taaluma la madini katika chuo cha madini,
One Stop centre Mirerani,
Brokers house Mirerani, uanzishwaji wa masoko ya madini mikoani, na uwekaji wa mfumo wa ulinzi wa kidigitali Mirerani, ununuzi wa mtambo wa uchorongaji miamba kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo kupitia STAMICO.
(xiii) Ardhi na Makazi: Kazi zilizotekelezwa ni pamoja na: kuandaliwa na kusajiliwa kwa Hati Milki 110,000 na Hati za Kimila 133,000; kuandaliwa kwa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 263 katika Wilaya 45; kuandaliwa kwa Mipango
Kabambe ya miji mikuu ya mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Mara, Singida, Iringa na Pwani, Ruvuma, Tabora na Simiyu; kuendelea na hatua za maandalizi ya Mipango Kabambe ya miji mikuu ya mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Rukwa, Shinyanga, Manyara, Dodoma, Tanga, Mbeya, Kagera, Kigoma, Katavi, Lindi, Kilimanjaro, Njombe na Geita; kuanzishwa kwa Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi; na kuongezeka kwa idadi ya benki na taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba kufikia 31 na kuwanufaisha wananchi 4,174. Aidha, Mfuko wa Mikopo Midogo Midogo ya Nyumba ulio chini ya Benki Kuu umeongezewa mtaji wa dola za Marekani milioni 18 ambapo taasisi za fedha tano (5) zimepatiwa mtaji wa shilingi bilioni 13.87 kwa ajili ya kukopesha wananchi wa kipato cha chini kwa masharti nafuu.
(xiv) Ujenzi wa Barabara Dar es Salaam: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya TAZARA (Mfugale flyover); kuendelea na ujenzi wa barabara za muingiliano Ubungo; mradi wa kuendeleza Jiji la Dar es Salaam km 210 za barabara kwa kiwango cha lami; na kuendelea na ujenzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara – Kibaha (km 19) kwa njia nane.
(xv) Ujenzi wa Meli: Hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na Ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika ziwa Victoria; kufikia asilimia 82 ya ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 za mizigo katika ziwa Nyasa; na kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili katika Ziwa Nyasa. Kwa upande wa Ziwa Tanganyika, Ujenzi wa Meli Mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo, ambapo uandaaji wa mikataba kwa ajili ya ujenzi wa meli hiyo pamoja na ukarabati wa meli ya MV Liemba umekamilika. Miradi mingine ni kukamilika kwa ujenzi wa kivuko kipya cha Kigongo – Busisi; kukamilika kwa ukarabati wa kivuko cha MV Pangani II; kuendelea kukarabati vivuko vya MV Sengerema, MV Kigamboni na MV Misungwi.
(xvi) Viwanja vya Ndege: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa asilimia 90.7 ya ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal III) katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere; kuendelea na upanuzi wa maegesho ya ndege, ujenzi wa jengo la mizigo, uzio wa kiwanja, maegesho ya ndege za mizigo na jengo la kuongozea ndege katika kiwanja cha ndege cha Mwanza. Aidha, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya mikoa vikiwemo vya Sumbawanga, Kigoma, Shinyanga, Mtwara, Songea, Mara, Songwe, Mbeya, Mwanza, Kigoma, Tabora na Iringa unaendelea.
(xvii) Mawasiliano: Hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo vituo vitatu (3) vya Mkongo katika maeneo ya Tukuyu, Kibaha na Kahama vimejengwa na kuvipa nguvu vituo vitatu (3) vya mkongo (Optical Line Amplifier (OLA) katika maeneo ya Ifakara, Kidatu na Mafinga; na kuendelea kutekeleza mradi wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi umetekelezwa kwa kubandika vibao vya namba za nyumba katika Halmashauri 12. Vile vile, Mfumo wa Usimamizi na Ufuatiliaji wa Mawasiliano ya Simu (TTMS) umekabidhiwa rasmi kutoka kwa Mkandarasi SGS/GVG ambapo katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Februari, 2019 jumla ya miamala 2,004,196,139 imepita katika mitandao ya simu na wastani wa fedha zilizopita ni Shilingi bilioni 12,202.7.
(xviii) Uendelezaji wa Bandari: Bandari ya Dar es Salaam: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi na kuanza kutumika kwa gati Na.1; na kuendelea na ujenzi wa sakafu ngumu katika gati la kupakua na kupakia magari;
Bandari ya Tanga: ukarabati wa miundombinu ya barabara kuelekea lango Na. 2 umekamilika;
Bandari ya Mtwara: ujenzi wa gati la mita 300 la kuhudumia shehena mchanganyiko unaendelea. Aidha, ujenzi wa Bandari katika Maziwa Makuu (Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa) unaendelea.
(xix) Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: kazi zilizofanyika ni kujengwa kilomita 140.42 za barabara kuu na kilomita 12.43 za barabara za mikoa kwa kiwango cha lami. Aidha, kwa upande wa madaraja hatua iliyofikiwa ni kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Mlalakuwa (Dar es Salaam); kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Momba (Rukwa) ambapo utekelezaji umefikia asilimia 94, Sibiti (Singida) asilimia 88.35, Mara (Mara) asilimia 85; na Ruhuhu (Ruvuma) asilimia 76; na kuanza ujenzi wa Daraja Jipya la Selander na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 5.2.
(xx) Ufungaji wa rada nne za kuongozea ndege za kiraia JNIA, KIA, Mwanza na Songwe: Hatua iliyofikiwa ni:
JNIA: Kukamilika kwa asilimia 95 ya miundombinu ya rada.
Mwanza: Ujenzi wa miundombinu ya rada unaendelea vizuri.
KIA: Ujenzi wa miundombinu ya rada unaendelea na umefikia asilimia 90.
Songwe: taratibu za ujenzi wa miundombinu zinaendelea. Aidha, mitambo itafungwa miundombinu itakapokamilika.
(xxi) Miradi ya Mahakama: Hatua iliyofikiwa ni: kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama za Wilaya za Bukombe, Chato, Ruangwa, Geita na Kilwa; kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo za Magoma (Korogwe) na Mlowo (Mbozi); kuendelea na ujenzi wa Mahakama za mikoa ya Njombe, Katavi, Lindi na Simiyu; kuendelea na ujenzi wa Mahakama za Wilaya za Kasulu, Sikonge, Kilindi, Bunda, Longido, Kondoa, Njombe, Rungwe, Chunya, Wanging’ombe, na Makete; kuendelea na ujenzi wa Mahakama Kuu Kigoma na Mara ambao umefikia asilimia 80; ujenzi wa Mahakama za Mwanzo za Mkunya (Newala), Uyole (Mbeya), Ngerengere, Mlimba na Mang’ula (Morogoro); ukarabati mkubwa wa nyumba tatu za kufikia Majaji Mtwara; na kukamilika kwa uboreshaji wa mfumo wa ukusanyaji takwimu na kusajili mashauri, kuingiza taarifa muhimu za wadaawa ikiwa ni pamoja na kutuma taarifa kwa ujumbe mfupi (sms) kwa wadaawa kuhusu mwenendo wa mashauri. Aidha, imeanzishwa huduma ya mahakama zinazotembea (mobile court, kwa kuanzia na mikoa ya Dar es salaam na Mwanza, magari ambayo yamezinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwezi Februari 2019.
(xxii) Miradi ya Kimkakati ya kuongeza mapato katika Halmashauri: Hatua iliyofikiwa ni utekelezaji wa miradi ya kimkakati 37 ya kuongeza mapato ya halmashauri na kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali ikijumuisha Soko la kisasa – manispaa ya Morogoro, soko la kisasa – halmashauri ya mji Kibaha, Pwani, ghala la kisasa – halmshauri ya wilaya ya Ruangwa, kituo cha mabasi Mbezi Louis – Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, soko la Mburahati – manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, ujenzi na upanuzi wa kiwanda cha kutengeneza chaki na kiwanda cha vifungashio – halmashauri ya wilaya ya Maswa, Simiyu, stendi ya mabasi Korogwe. Miradi hii inatekelezwa katika halmashauri 29 na ipo katika hatua mbalimbali.
(xxiii) Uwekezaji: Sekta ya Uwekezaji imeendelea kukua ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo ripoti mbalimbali za uwekezaji duniani zinaonesha Tanzania imeongoza kwa kuvutia uwekezaji kati ya nchi za Afrika Mashariki. Kwa mfano, Ripoti ya Uwekezaji ya Dunia ya mwaka 2018 inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) inaonesha kuwa Tanzania imevutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 1,180, ikifuatiwa na Uganda Dola za Kimarekani milioni 700 na Kenya Dola za Kimarekani milioni 672. Aidha, ripoti ya “Where to Invest in Africa” ya mwaka 2018 inayojulikana kama
RMB’s Investment Attractiveness Index inayoonesha nchi zinazovutia zaidi kwa uwekezaji barani Afrika, Tanzania imeendelea kuwa katika kumi bora kwa kushika nafasi ya saba (7) kati ya nchi 52 ikipanda kutoka nafasi ya 9 mwaka 2017.
Aidha, jitihada za Serikali kuhamasisha ujenzi wa viwanda nchini zimewezesha kuongezeka mitaji katika viwanda mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mtaji uliowekezwa chini ya Mamlaka ya EPZ umeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.422 mwaka 2016 hadi Dola za Marekani bilioni 2.23 hapo Novemba, 2018, ikiwa ni ongezeko la Dola za Marekani milioni 808 (sawa na ongezeko la asilimia 56.8). Mwenendo wa mauzo ya bidhaa za viwanda hivyo nje ya nchi yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.194 hapo Novemba 2018, kutoka Dola za Marekani bilioni 1.1 mwaka 2016, ikiwa ni ongezeko la asilimia 99.45. Mtaji mkubwa umewekezwa katika viwanda vya kuongeza thamani mazao (agro processing) ambapo ina asilimia 38 ya mtaji wote; zikifuatiwa na viwanda vya kuunganisha mitambo (assembling & engineering) asilimia 31 ya mtaji, mavazi na nguo asilimia 21 ya mtaji na uchakataji madini asilimia 10 ya mtaji. Aidha, viwanda 71 ni vya makampuni ya kigeni, viwanda 58 ni vya makampuni ya ubia na viwanda 45 ni vya makampuni ya ndani.
(xxiv) Kuhamishia Utekelezaji wa Majukumu ya Serikali Makao Makuu Dodoma: Serikali imetekeleza azma yake ya kuhamia Makao Makuu ya Nchi, Dodoma ambapo mpaka hivi sasa Wizara zote zimeshahamia Dodoma na jumla ya Watumishi 8,883 wanatekeleza majukumu yao wakiwa hapa Dodoma (Watumishi hao ni kutoka Ofisi/Wizara na Vyombo vya Ulinzi na Usalama). Vile vile, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri pia wameshamia Dodoma. Uendelezaji wa eneo la Mji wa Serikali – Ihumwa umeanza na jumla ya majengo 22 ya Ofisi za Wizara na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yako katika hatua za mwisho za ujenzi.
(xxv) Mfuko wa Maendeleo ya Vijana: Serikali imeendelea kuwawezesha Vijana kiuchumi ili waweze kujiajiri katika nyanja za uzalishaji mali na kutoa huduma ambapo hatua iliyofikiwa ni: kutolewa kwa mikopo nafuu yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.74 kwa vikundi vya vijana 523, vyenye wanachama 3,661 katika Halmashauri 128 za Tanzania Bara; na kuanzishwa kwa SACCOS 127 za Vijana kati ya 184 zinazotarajiwa kuanzishwa hadi kufikia mwaka 2020.
(xxvi) Mafanikio mengine ni kuendelea kuimarika kwa
Amani, utulivu na usalama nchini hivyo, kuwezesha kukua kwa shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika kutimiza jukumu hilo, Jeshi la Polisi limeendelea kuweka juhudi katika kudhibiti uhalifu sanjari na kuendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili jamii ibadilike na kuachana na matukio ya uhalifu.
(xxvii) Mazingira: Serikali imetekeleza hughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa ikolojia ili kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, kujenga uwezo w taasisi na jamii kuhimili changamoto za mazingira na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuboresha kanuni za kutoa leseni za tathmini ya mazingira kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa leseni za muda kabla ya kuanza mradi.
(xxviii) Miradi ya Sekta Binafsi: Sekta hii imeendelea kushiriki katika ujenzi wa viwanda ambapo katika kipindi cha 2015 hadi 2018, jumla ya viwanda 3,530 vilijengwa na kuanza uzalishaji.
- MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2019/20
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20 ni wa nne katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21, wenye dhima ya Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo ya Watu. Maandalizi ya Mpango huu yamezingatia azma ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; na Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 yanatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambavyo ni:
(i) Viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda: Miradi itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususan kilimo, madini na gesi asilia. Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia, Uanzishwaji na Uendelezaji wa Kanda Maalamu za Kiuchumi
na Kongane za Viwanda, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza thamani ya madini na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu;
(ii)
Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, elimu na ujuzi, upatikanaji wa chakula na lishe bora na huduma za maji safi na salama. Shughuli zitakazotiliwa mkazo ni pamoja na kugharamia utoaji wa elimu msingi bila ada, kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu), ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi nchini, kuboresha huduma za maji vijijini;
(iii) Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji: Miradi itakayotekelezwa katika eneo hili ni ile yenye lengo la kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu (reli, bandari, nishati, viwanja vya ndege, barabara). Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji Rufiji MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha
Standard Gauge; na kuendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na Uwekezaji. Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 umeweka msukumo katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza ikiwemo kupitia upya mfumo wa kitaasisi, kisera na kisheria pamoja na kanuni zake ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo; na
(iv)
Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango: Miradi inayotekelezwa katika eneo hili inalenga kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji wa Mpango, kuweka mfumo utakaowezesha upatikanaji wa uhakika wa rasilimali fedha na kuweka vigezo vya upimaji wa mafanikio ya utekelezaji.
SEHEMU YA TATU
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19 NA MAPENDEKEZO YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2019/20
- TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19
- Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018/19, Serikali ilipanga kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 32,476.0. Kiasi hicho kinajumuisha: mapato ya ndani shilingi bilioni 20,894.6; misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo shilingi bilioni 2,676.6; na mikopo yenye masharti ya kibiashara kutoka vyanzo vya ndani na nje shilingi bilioni 8,904.7. Aidha, matumizi ya kawaida yalikadiriwa kuwa shilingi bilioni 20,468.7 na matumizi ya maendeleo shilingi bilioni 12,007.3.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 9,111.9, mapato yasiyo ya kodi shilingi bilioni 1,522.9 na mapato yaliyokusanywa na Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 371.7.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kama ilivyoainishwa ndani ya Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na Uwekezaji (Blueprint) kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato ya Serikali. Hatua hizo ni pamoja na: Kupunguza kodi kwa wachimbaji wadogo wa madini; Ugawaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wadogo; Kupunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa unaotozwa kwenye pombe kali zinazotengenezwa nchini kwa kutumia zabibu zinazozalishwa nchini; Kuweka utaratibu mpya wa ukusanyaji wa kodi ya majengo; Kuboresha mifumo ya TEHAMA ya kukusanya kodi na maduhuli ikiwemo Electronic Fiscal Device Management System (EFDMS) ambao hupokea na kutunza kumbukumbu za utoaji wa risiti za mauzo.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Januari 2019, Washirika wa Maendeleo walitoa jumla ya shilingi bilioni 1,034.8. Kati ya kiasi kilichotolewa, misaada na mikopo nafuu ya Kibajeti ilikuwa shilingi bilioni 125.4 na miradi ya maendeleo shilingi bilioni 782.0. Mifuko ya Kisekta ilipokea shilingi bilioni 127.4.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, Serikali ilikopa shilingi bilioni 2,025.0 kutoka soko la ndani. Aidha, katika kipindi hicho, Serikali ilifanya majadiliano na taasisi mbalimbali za kifedha za kimataifa na kupata shilingi bilioni 458.6 kutoka Benki ya Credit Suisse mwezi Februari 2019 na shilingi bilioni 247.7 zinatarajiwa kupatikana kutoka benki ya HSBC hivi karibuni. Vile vile, Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na baadhi ya wakopeshaji walioonesha nia ya kuikopesha Serikali kwa mwaka 2018/19.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi ya jumla ya shilingi bilioni 13,750.6. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 10,962.1 zilitolewa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi bilioni 2,788.5 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Mahitaji yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa fedha ni pamoja na: Ulipaji wa deni la Serikali ikijumuisha michango ya mwajiri katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii shilingi bilioni 5,465.9 ambapo Shilingi bilioni 3,803.4 zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo; na mishahara ya watumishi wa Serikali shilingi bilioni 3,890.0. Serikali imeshatenga na inatarajia kutoa kiasi cha Shilingi bilioni 1,433.8 kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo mradi wa kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji Mto Rufiji (MW 2,115).
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ili kufikia malengo ya bajeti ya mwaka 2018/19. Miongoni mwa mikakati hiyo ni: Kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari kupitia vipindi mbalimbali vya elimu kwa umma; Kutekeleza mwongozo wa ushirikiano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo; Kuendelea kusisitiza nidhamu ya matumizi katika utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya Mwaka 2015; kulipa madai yote yaliyohakikiwa ya makandarasi; Kuanza kutumika kwa Mfumo wa Kielektroniki wa Stampu za kodi (ETS) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi; na Kutekeleza Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS) ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa makusanyo ya kodi za ndani.
- SERA ZA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/20
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera za mapato kwa mwaka 2019/20 zitalenga: Kuboresha mazingira ya kufanya biashara ili kuvutia uwekezaji, ukuaji wa biashara ndogondogo na za kati pamoja na ukuaji wa uchumi endelevu; Kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari, upanuzi wa wigo wa kodi na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika usimamizi wa kodi; Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; Kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wakala za Serikali na Mamlaka za Udhibiti; na Kuwajengea uwezo maafisa wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala na Halmashauri ili kuimarisha uwezo wa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa mazingira haya utawezesha kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa uwekezaji, uzalishaji, ajira na miamala ya biashara ambayo kwa ujumla itachangia kuongezeka kwa vyanzo vya mapato. Aidha, kwa upande wa misaada na mikopo nafuu, Serikali itaendelea kuimarisha mahusiano kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Ushirikiano na Washirika wa Maendeleo.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2019/20, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, SURA 439. Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi mikubwa ya miundombinu na miradi mingine muhimu. Aidha, Serikali itaendelea kugharamia matumizi ya maendeleo yenye vyanzo mahsusi kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo maalum yenye maslahi mapana kwa Taifa kama vile Mfuko wa Barabara, Mfuko wa Reli, Mfuko wa Nishati Vijijini na Mfuko wa Maji. Vile vile, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la madeni ya Serikali.
- Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka 2019/20
- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia sera za bajeti kwa mwaka 2019/20, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya Shilingi bilioni 33,105.4 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika ambapo mapato ya ndani, yakijumuisha mapato ya halmashauri, yanatarajiwa kuwa Shilingi bilioni 23,045.3. Mikopo ya ndani inakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 4,960.0, mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi bilioni 2,316.4 na misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo Shilingi bilioni 2,783.7.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2019/20 Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 33,105.4 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 20,856.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida; matumizi haya yanajumuisha gharama za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020. Matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa shilingi bilioni 12,248.6, ambapo shilingi bilioni 9,737.7 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 2,510.9 ni fedha za nje.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka 2019/20 ni kama ilivyo katika Jedwali lifuatalo:
........
HITIMISHO
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango na Bajeti ya mwaka 2019/20 unazingatia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano chini na uongozi thabiti wa Mheshimwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha ustawi wa jamii. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi. Vile vile, Serikali itaendelea kuweka mkazo katika usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ili zitumike katika uwekezaji wa miundombinu ya umma na uboreshaji wa huduma za kijamii kwa lengo la kuleta maendeleo ya haraka. Hivyo, napenda kuwahimiza Watanzania tuwajibike kulipa kodi na kuhakikisha tunatoa na kudai risiti kulingana na muamala uliofanyika.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa, kuimarisha ulinzi wa rasilimali za umma na kudhibiti matumizi ya fedha za umma. Serikali pia itaongeza msukumo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara na Uwekezaji. Mpango huu, pamoja na mambo mengine, unakusudia kuhuisha na kurahisisha taratibu za kulipa kodi, tozo na ada mbalimbali.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.