Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 2,131.57 kwa mwaka 2016 hadi kufikia Dola za Marekani 2,250.3 kwa mwaka 2017 ikiwa ni sawa na asilimia 5.6.
Hayo yameelezwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa MaliAsili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019.
"Idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka kutoka watalii 1,284,279 kwa mwaka 2016 hadi kufikia watalii 1,327,143 kwa mwaka 2017, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.3. Watalii kutoka Marekani wameongoza katika kuitembelea Tanzania wakifuatiwa na nchi za Uingereza, India, Uholanzi na Uswisi," amesema Dkt. Kigwangalla.
Ameendelea kusema, mafanikio hayo yanatokana na ujenzi wa miundombinu ya barabara, kuongezeka kwa kasi ya kuboresha na kutangaza vivutio vya utalii, kuimarishwa kwa mifumo ya ukusanyaji madhuhuli na kudhibiti matukio ya ujangili na matumizi yasiyo endelevu ya maliasili na malikale.
Vile amesema, katika juhudi za kutangaza utalii, Wizara imeendelea kutekeleza mikakati mabalimbali ikiwemo kuandaa utambulisho wa Tanzania Kimataifa (Destination Branding). Lengo ikiwa ni kuitambulisha Tanzania kama kituo mahsusi cha utalii Duniani.
Aidha, Wizara hiyo inashirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kuanzisha chaneli maalum katika Televisheni ya Taifa (TBC 1) kwa ajili ya kutangaza utalii ambapo kwa sasa Wizara inaendelea na maandalizi ya kuanzisha studio ya kutangaza utalii kwa njia ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Pia amesema, Wizara imeanza kutengeneza mfumo mmoja funganishi wa TEHAMA unaoitwa "MNRT Portal" kwa kutoa leseni na vibali, ukusanyaji wa takwimu na mapato kutoka vyanzo mbalimbali vya sekta ya Maliasili na Utalii.
"Mfumo huo utaunganishwa na mfumo wa Serikali wa malipo ya kielektroniki na kuhuishwa na mifumo mingine ya Serikali kama vile Uhamiaji, NIDA, TIRA, BRELA, TRA na NBS. Mfumo huo utaiwezesha Wizara kufuatilia watalii wa nje na wa ndani, kukusanya na kuchambua takwimu za sekta ya maliasili na utalii kwa wakati, kuimarishsa utoaji wa huduma kwa wateja na kufanikisha ukusanyaji udhibiti wa mapato," amesema Dkt. Kigwangalla.
Mfumo huo ambao utatumiwa na Wizara, Taasisi na wadau mbalimbali unatarajia kuanza kutumika rasmi mwaka ujao wa fedha.
Wakati huohuo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Nape Nnauye ameipongeza Serikali kwa kuboresha miundombinu ya utalii hususan barabara, huduma za maji na umeme ambavyo vimeendelea kuvutia watalii wengi kutembelea vivutio vya utalii na kuongeza idadi ya watalii hapa nchini.
"Kamati inaipongeza Serikali kuwezesha kujengwa kwa uwanja wa ndege wa Chato Uwanja huu utasaidia kufungua fursa nyingi za utalii hasa vivutio vilivyopo katika kanda za ziwa. Vivutio hivyo ni pamoja na Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda, Rumanyika, Hifadhi za Taifa za Saanane na Rubondo," amesema Mhe. Nape.
Amesema, ili kuupa thamani uwanja wa ndege wa Chato ni muhimu Serikali ikawekeza vya kutosha katika kuviendeleza vivutio vya utalii vya ukanda huo, kujenga na kuimarisha miundombinu ya barabara, maji, umeme pamoja na kuvutia wawekezaji kujenga mahoteli ili kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea vivutio hivyo katika kanda ya ziwa.
Wizara ya MaliAsili na Utalii imeliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi Bilioni 115,794,740,000 kwa matumizi ya fungu 69 - Wizara ya MaliAsili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Kati ya fedha hizo shilingi 85,816,658,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 29,978,082,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.