Na Tiganya Vincent
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu anatarajia kufanya ziara rasmi ya siku tano kuanzia kesho tarehe 21 hadi 26 Februari , 2019 mkoani Tabora.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari ofisini kwake.
Alisema Makamu wa Rais anatarajiwa kuwasili Mkoani Tabora kupitia Wilaya ya Igunga ambapo atapata taarifa ya Mkoa na kisha kuongea na watumishi na viongozi mbalimbali.
Mwanri alisema kuwa akiwa wilayani Igunga ataweka jiwe la Msingi katika miradi ya maendeleo ikiwemo maji na afya katika upanuzi wa Kituo cha Afya Simbo na kuwahutubia wananchi.
Aliongeza kuwa kesho yake Februari , 22 Makamu wa Rais atapokea taarifa ya miradi ya Wilaya ya Nzega na kisha ataweka jiwe la Msingi ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega.
Mwanri alisema kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa wodi katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega ataweka jiwe la msingi ujenzi wa kiwanda cha Gesi na baadae atawahutubia wakazi wa Nzega katika Viwanja vya Puge.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema siku hiyo hiyo , Makamu wa Rais atawasili wilayani Uyui ambapo atapokea taarifa ya miradi mbalimbali na kisha ataweka jiwe la Msingi ujenzi wa Kituo cha Afya Igalula na baada ya shughuli hiyo Makamu wa Rais atawahutubia wananchi wa Igalula.
Mwanri aliongeza kuwa mnano Februari 23, 2019, Makamu wa Rais atapokea taarifa ya miradi na kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na kuwahutubia wakazi wa Sikonge mjini katika Viwanja vya TASAF.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa Februari 24, 2019 atapokea taarifa ya miradi na kufungua chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Kaliua, baada ya hapo ataweka Jiwe la Msingi ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Kaliua na kisha atawahutubia wananchi katika Uwanja wa Kolimba.
Mwanri alisema mchana ataelekea wilayani Urambo ambapo atapokea taarifa ya miradi na kuweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ussoke Mlimani na kuwahutubia wananchi.
Alisema mnamo Februari 25, 2019, Makamu wa Rais atapokea taarifa ya miradi ikiwemo ya upandaji miti na kuweka jiwe la msingi katika upanuzi wa Kituo cha Afya cha Maili Tano na kuwahutubia wakazi wa Manispaa ya Tabora katika Viwanja vya Chipukizi.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa wakazi wote wa Mkoa wa Tabora kujitokeza kwa wingi kumlaki na kumsikiliza na kupokea maagizo ambayo Makamu wa Rais atatupatia kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wao.