Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) linalojengwa na Kampuni ya Ujenzi ya Suma JKT katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu alitembelea mradi huo na kuonesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa mkandarasi aliyekuwa akijenga jengo hilo ambaye ni Wakala Majengo Tanzania (TBA) na kuagiza kuvunjwa kwa mkataba.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Mei 13, 2020) wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la NEC. Amesema amefurahishwa na hatua iliyofikiwa na anaamini litakamilika kwa wakati.
“Ninahakika mkiongeza nguvu katika baadhi ya maeneo tutafika na haya ndio Serikali inataka kuona taasisi zake zikifanya. Kwenye jengo hili ndipo Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuchukua fomu.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya Ujenzi ya Suma JKT kwa namna walivyoratibu vizuri ujenzi wa jengo hilo. “Miradi mingi waliyokabidhiwa Suma JKT imekuwa ikijengwa kwa weledi mkubwa.”
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenyeulemavu, Jenista Mhagama amesema Kampuni ya Ujenzi ya Suma JKT ilikabidhiwa mradi wa ukamilishaji wa jengo hilo Desemba 24, 2019 na unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2020.
Amesema mradi huo unaosimamiwa na Chuo Kikuu Ardhi (ARU) kama mshauri wa mradi hadi leo (Mei 13, 2020) ujenzi wa jengo kuu la ofisi umefikia asilimia 85, jengo la kutangazia matokeo ujenzi wake umefikia asilimia 68, kazi za nje zimefikia asilimia 85 huku jengo la ghala limefikia asilimia 92.
Naye, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera amesema mkataba wa mradi huo ulipaswa ukamilike Aprili 30, 2020 lakini baada ya kutembelea eneo la mradi wamekubaliana kuwa kazi hiyo iwe imekamilika ifikapo Mei 30, 2020 na Juni 1, 2020 watumishi wahamie na kuanza kazi.
Amesema mradi huo unagharimu zaidi ya sh. bilioni 12 na tayari zaidi ya sh bilioni sita zimeshatolewa na kwamba kazi zinazoendelea kwa upande wa jengo kuu la ofisi ni pamoja na kupachika milango na madirisha, kupaka rangi na kuweka vigae kwenye sakafu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA,
JUMATANO, MEI 13, 2020.