Amesema mipango maalumu itakayoandaliwa na mifuko inayotoa dhamana kwa wafanyabiashara na wajasiriamali inatakiwa iwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na baadaye taarifa za utekelezaji zitolewe katika kipindi cha kila robo mwaka.
“Wasimamizi na Watendaji wa mifuko na programu pamoja na walengwa jiepusheni na vitendo vya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki na ni kikwazo kikubwa cha maendeleo. Pia, watendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji pamoja na taasisi za fedha hakikisheni mnatoa huduma bila urasimu wala ubaguzi wa aina yoyote. Nasisitiza wananchi wanapofika kwenye ofisi zenu wapokelewe kwa staha, wasikilizwe na kupatiwa huduma stahiki kwa wepesi.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoawito kwa vyombo mbalimbali vya habari kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo ili viweze kufikisha ujumbe sahihi kuhusu fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mifuko na programu za uwezeshaji kwa wananchi wote nchini.
Waziri Mkuu amesema tathmini za mara kwa mara zinazofanywa na Serikali kuhusu utendaji wa Mifuko na Program za Serikali za uwezeshaji zinaonesha kwamba mifuko hiyo na programu hizo zimechangia kwa kiwango kikubwa jitihada zake za kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
“Takwimu zinaonesha kwamba katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 mifuko na programu za uwezeshaji za Serikali zimefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 2.22 na hivyo, kunufaisha zaidi ya watu milioni 4.9 na taasisi 5,499.”
Waziri Mkuu amesema sambamba na programu na mifuko hiyo, Halmashauri 185 Tanzania Bara zimefanikiwa kutoa shillingi bilioni 93.3 kupitia mifuko ya uwezeshaji wa makundi maalum ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Fedha hizo, zimewezesha upatikanji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi 32,553.
“Nitumie nafasi hii kuendelea kusisitiza kwamba kila Halmashauri ihakikishe inatenga asilimia 10 ya mapato yake ya fedha za ndani ili zitumike kutoa mikopo kwa vijana (asilimia 4), wanawake (asilimia 4) na watu wenye ulemavu (asilimia 2). Pia, natoa wito kwa Mabaraza ya Madiwani katika kila Halmashauri kufuatilia utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali ambayo yameridhiwa na Bunge na kutungiwa sheria mahsusi.”
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa amesema baraza hilo linajukumu la kusimamia, kufuatilia na kuratibu shughuli mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiwemo mifuko na programu za uwezeshaji.