Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Elikana Balandya awasimamishe kazi watumishi wawili wa Jiji la Mwanza huku akiagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa huo arudishwe wizarani na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Ameagiza ujenzi wa ghorofa uliositishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Amos Makalla uendelee kwenye viwanja namba 194 & 195 kitalu ‘U’ Rwagasore, jijini Mwanza na wamiliki wa viwanja hivyo wakabidhiwe hati zao kama alivyokuwa ameelekeza awali.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Oktoba 3, 2023) kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo.
“Ninaagiza Katibu Tawala wa Mkoa wasimamishe kazi Mkuu wa Idara ya MipangoMiji, Bw. Robert Phares na Afisa Mteule na Mkuu wa Kitengo cha Ardhi katika Jiji la Mwanza, Bi. Halima Iddi Nasoro. Na Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi (Mwanza), Bw. Elia Kamihanda arudishwe makao makuu na achukuliwe hatua za kinidhamu.’’
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wawafuatilie na kuwarejesha Dodoma watumishi 11 waliokuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili wajibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, kupora maeneo ya wananchi na kugawa maeneo ya wazi.
"Watumishi wa Jiji la Dodoma ni Josephat Mafuru (aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji), Scorpion Philip, Lennis Ngole, Allen Mwakanjuki, Aisha Masanja, Agusta Primo, Azory William Byakanwa, Frezia Kazimoto, Premin Nzenga, Stella Komba na Thabiti Mbiyagi. Hawa ni wachache miongoni mwa wengi waliohusika kusababisha migogoro, watafutwe na waje kujibu tuhuma dhidi yao," amesema.
Amesema kuwa Jiji la Dodoma litekeleze mapendekezo ya Kamati Maalum ya Uchunguzi kwa kufanya uhakiki wa hati pandikizi zote, litafute maeneo na kuwafidia wananchi wanaolidai Jiji na liwe limekamilisha utekelezaji ifikapo Januari 30, 2024. “Halmashauri ya Jiji isitishe upimaji shirikishi wa asilimia 70 kwa 30 na sasa wabaini wananchi wote waliohusika na zoezi hilo ili walipwe ifikapo Januari 30, 2024.”
Ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi wajiridhishe kuhusu matumizi ya fedha za Mkopo wa Mradi wa KKK sh. bilioni moja zilizotumika kulipa fidia ili kupisha upanuzi wa ujenzi wa hoteli ya Jiji (Dodoma City Hotel) iliyoko mtaa wa Uhindini.
Ameagiza maeneo yote ya umma ikiwemo shule, vituo vya afya, bustani za kupumzikia na masoko, yasibadilishwe matumizi yake hadi yaidhinishwe na Kamati za Usalama za Wilaya na Mikoa kama ipo haja ya kufanya hivyo na kuridhiwa na Waziri wa Ardhi, baada ya kupokea muhtasari wa Kamati ya Usalama ya Mkoa.
Pia ameagiza OR - TAMISEMI na Wizara ya Ardhi wafute hati zote zilizopimwa kwenye Bonde la Makutupora na kuwaondoa wavamizi waliojenga kwani hicho ni chanzo cha maji.
Awali, katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (SBU), Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, OR - TAMISEMI na Ardhi, Wakuu wa Mikoa hiyo sita, Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Majiji hayo, Kamati Maalum ya Uchunguzi iliyoundwa na Waziri Mkuu ilibainisha kuwa mradi wa upimaji shirikishi wa asilimia 70 kwa 30 ulikuwa ni dhana iliyokuwa inatumiwa bila kufuata sheria.
“Upimaji shirikishi haukuwa na msingi wa kisheria bali Halmashauri walitumia mikataba baina yao na makampuni ya upimaji. Mwananchi hakuingia mkataba na Jiji isipokuwa katika eneo la Nkuhungu peke yake. Halmashauri hiyo ilikuwa inatoa muda wa siku 90 kwa mwananchi kulipia eneo alilopatiwa na akishindwa kulipia ndani ya muda huo, alikuwa akinyang'anywa eneo lake,” alisema mjumbe wa Kamati hiyo.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji anatuhumiwa kutumia sh. bilioni 3 zilizokopeshwa na Wizara ya Ardhi kupima maeneo mapya na kulipa fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao. “Oktoba 11, 2021 Mkurugenzi aliomba sh. bilioni 5.95 ili zitumike kupima ardhi na kumilikishwa mashamba ndani ya Jiji katika maeneo ya Zuzu na Bihawana. Januari 2022, walipata mkopo wa sh. bilioni 3 na walitakiwa kuurejesha ndani ya miezi sita. Hadi Julai, 2023 Jiji la Dodoma lilikuwa imerejesha milioni 962 na bado inadaiwa sh. bilioni 3.93.”
Watumishi wengine wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuuza viwanja kwa zaidi ya mtu mmoja (double allocation), kutumia fedha za miradi kinyume na taratibu, kutoa kazi za upimaji kwa kampuni binafsi bila kufuata taratibu, kughushi hati za viwanja na kuuza maeneo ya wazi kwa matumizi binafsi.