Na Munir Shemweta, WANMM BUKOMBE
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula ameziagiza idara za ardhi kwenye halmashauri kuhakikisha maeneo yanayotengwa kwa ajili ya shughuli za uwekezaji yanapimwa sambamba na kuwa na mpango wa matumizi bora ardhi katika vijiji.
Dkt. Mabula alisema hayo jana wilayani Bukombe akiwa katika ziara yake ya kikazi kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na kukagua miradi inayejengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mkoa wa Geita.
Alisema kuna baadhi ya maeneo kwenye halmashauri nchini yametengwa kwa ajili ya shughuli za uwekezaji lakini hayajapimwa huku baadhi ya vijiji vikiwa havijawekewa hata mipango ya matumizi bora ya ardhi jambo alilolieleza linaweza kuwakimbiza wawekezaji na kuleta migogoro ya ardhi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, wakati wa mchakato wa kutenga maeneo ya uwekezaji ndani ya halmashauri, ni vizuri utengaji maeneo hayo ukaenda sambamba na kuyapima maeneo hayo huku juhudi zikiongezwa kuviwekea vijiji mipango ya matumizi bora ya ardhi.
“Asije muwekezaji ndiyo muanze zoezi la uhaulishaji, ni vizuri kuyapima maeneo hayo ya uwekezaji kwa kuwa suala la uhaulishaji linaweza kuchukua muda na linataka idhini ya Rais”, alisema Dkt. Mabula
Naibu Waziri wa Ardhi ambaye katika ziara yake hiyo alitembelea pia halmashauri za wilaya za Chato na Geita na kuziagiza halmashauri kuongeza kasi katika uwekeji mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji sambamba na kuvipatia vyeti ili kuondokana na migogoro ya mara kwa mara hasa ile ya wakulima na wafugaji.
Katika taarifa yake kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani Geita ilieleza kuwa imeandaa na kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vitano vya Kagwe, Kidete, Bukombe, Ilalwe na Nasihukulu kwa kushirikiana na Timu ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi Taifa.
Akigeukia utendaji kazi wa ofisi za ardhi za mikoa zilizozinduliwa hivi karibuni, Dkt Mabula alizitaka halmashauri kuzitumia ofisi hizo katika shughuli mbalimbali za masuala ya ardhi hata pale ambapo kuna upungufu wa watumishi pamoja na ukosefu wa vifaa.
Alisema, halmashauri kushindwa kuzitumia ofisi za ardhi za mikoa katika masuala mbalimbali ya ardhi kama vile upimaji haitakuwa na maana ya kuzianzisha ofisi hizo ambazo jukumu lake kubwa ni kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi.