Na .Tiganya Vincent-RS-TABORA
KAMATI ya Ulinzi na Usalama mkoani Tabora imezuia vifaa vya ujenzi vya Kampuni ya Ceytun iliyokuwa ikipanua Uwanja wa Ndege na kuwang’anywa hati za kusafiria za viongozi wake wawili hadi watakapomalizia malipo ya waliokuwa wafanyakazi wao.
Uamuzi huo umetolewa jana mjini Tabora na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alipokuwa akitoa maamuzi ya wajumbe wake kwenye mkutano na viongozi wa Kampuni hiyo na wanaodai.
Alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya Mhasibu wa Kampuni hiyo Bw. Mahmut Garik kukataa kutoa vielelezo vinavyoonyesha jinsi alivyowalipa waliokuwa wafanyakazi wao ili kuona kama madai ya wafanyakazi hao ni halali au sio halali.
Mwanri alisema kuwa zoezi la kushughulikia madai ya wafanyakazi hao ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipotembelea Uwanja wa Ndege mkoani Tabora kuonyeshwa bango la kumdai mmiliki wa Kampuni na ndipo Rais aliagiza lishughulikiwe.
Alisema kuwa wakati wa majadiliano baina ya pande zote tatu yakiendelea na ndipo Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora alipomwomba Mhasibu wa Kampuni hiyo kuwasilisha vielelezo vinavyoonyesha ushahidi wake kama kweli alisha walipa wafanyakazi wake na ndipo alipojibu kuwa hawezi kutoa labda waendee Mahakamani.
“Kitendo hicho cha kuonyesha jeuri hakiwezi kukubalika…RPC hakikisha hatoi vifaa vyake na Uhamiaji chukua Hati zao za kusafiri …hadi ukweli ujulikane…maana wakishaondoka Tabora wananchi hawa hawawezi kuwapata” alisema Mwanri
Kwa upande Meneja Mradi wa Kampuni ya Ujenzi ya Ceytun Ercan Kavaic aliomba radhi kwa kauli ya Mhasibu wake ya kukataa kutoa nyaraka hizo ambazo ndio zingesaidia kuondoa mvutano huo.
Aliahidi kukaa pamoja na wadai wake na watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kupitia madai na kuna njia bora ya kutatua tatizo hilo.
Kavaic alikubali vifaa vyake kuwa chini ya ulinzi na kutoa hati yake ya kusafiria hadi hapo watakapopata muafaka.
Kwa upande wa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tabora Damian Ndabalinze aliwashauri vijana wanaomba kazi katika Kampuni mbalimbali za ujenzi wakahakikisha wanapewa mikataba kabla mradi haujaanza ili wajue malipo na stahili wanazopaswa kupata ili kuondoa migogoro wa malipo pindi wanapokuwa wamemaliza mkataba.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Wilbroad Mtafungwa alimwakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa hakuna kifaa kitakachoondoa katika eneo la mradi hadi hapo wakapokuwa wamehakikishiwa kuwa mgogoro ulipo wa malipo umemalizika.