Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Serikali kuwachukulia hatua maafisa utumishi watakaochelewesha upandaji wa madaraja pamoja ulipaji wa ongezeko la mishahara kwa watumishi wa Umma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora Mhe. Angellah Kairuki ametoa tamko hilo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali juu ya ucheleweshaji wa upandaji wa madaraja kwa watumishi wa Umma.
“Watumishi wa Umma 193,000 watapandishwa madaraja mwaka huu wa fedha, aidha watumishi wote wanaostahili kupandishwa madaraja watapandishwa,” amefafanunua Mhe. Angellah Kairuki.
Ameeleza kuwa, kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya ofisi za Serikali juu ya ucheleweshaji wa upandishaji wa madaraja pamoja na ulipaji wa nyongeza za mishahara.
Hivyo basi, amewataka maafisa utumishi wote nchini kupandisha madaraja watumishi wao kwa wakati, aidha Serikali itamchukulia hatua au kusimamisha mshahara kwa Afisa utumishi atakayezembea kupandisha madaraja kwa watumishi wake.
Hata hivyo, Angellah Kairuki amewatoa hofu watumishi wa Umma juu ya ongezeko la mwaka la mshahara na kusema kuwa muda wowote ndani ya mwaka huu wa fedha watumishi hao wataongezewa ongezeko hilo katika mishahara yao.
Katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Trilioni 1 kwa ajili ya ulipaji wa madeni ya watumishi wa Umma na wazabuni mbalimbali wanaoidai Serikali.
Juni, 2016 Serikali ilisitisha ajira na upandaji wa madaraja kwa watumishi wote wa Umma ili kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.