Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Lukuvi Ayataka Mabenki Kutowaonea Wanyonge Kwa Njia ya Mikataba
Sep 01, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_11368" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Ardhi, Nymba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (Picha na Mtandao)[/caption]

Na: Jonas Kamaleki 

Mabenki na Taasisi nyingine za fedha zimetakiwa kuandika mikataba yake kwaa wateja kwa lugha rahisi na ya Kiswahili ili kuepusha usumbufu wanoupata wakopaji bila kujua masharti ya mikopo.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi alipokuwa akizungumza katika kikao kazi cha kubaini na kutatua changamoto za mabenki , na wenyeviti wa mabaraza ya ardhi nchini.

Akifafanunua kuhusu usumbufu wanoupata wakopaji, Lukuvi amesema masharti ya mkopo yawekwe wazi kwa mkopaji kabla ya kupewa mkopo. Ameongeza kuwa kinyume chake mtu anapewa mkopo kwanza ,  masharti na taratibu nyingine za mkopo zinatolewa baadae.

Ametoa mfano kuwa mteja anaambiwa kuwa mkopo wake riba yake ni aslimia 8 kwa mwezi, mteja bila kujiuliza na kwa sababu fedha anaihitaji anasema sawa kumbe kwa mwaka anajikuta analipa riba kubwa.

Waziri Lukuvi amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa benki wasio waaminifu kuwasababishia wateja wao usumbufu mkubwa pindi wanaposhindwa kurejesha mkopo. Amesema biashara hiyo ife mara moja.

“Ninafahamu baadhi yenu ninyi watu wa benki mnashirikiana na madalali kunadi nyumba za watu kwa kisingizio cha kushindwa kulipa mkopo huku mkizinunua wenyewe kwa viwango mnavyotaka, hiyo tabia si nzuri mkibainika hatua stahiki zitachuliwa dhidi yenu”alisema Lukuvi.

Ameongeza kuwa katika utafiti wake ndani ya kipindi cha miezi mitatu takribani nyumba 180 zimeuzwa na kubadilishwa umiliki kwa ajili ya watu kushindwa kulipa mikopo yao. Amesema hali hii si ya kawaida na Dar es Salaam ndiyo inaongoza kwa vitendo hivyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Mabenki Tanzania, Tusekilege Mwaikasu amesema wanaafiki rai ya Waziri ya kuandaa mikataba na wateja kwa Kiswahili ili kuwapa nafasi wateja wao kufahamu undani wa mikataba hiyo.

Kuhusu mashauri ya wateja ambayo yapo kwenye mabaraza ya ardhi na vyombo vingine vya sheria ni zaidi ya 2000 ambayo thamani yake ni sawa na bilioni 20 fedha ya kitanzania. Ameongeza kuwa hali hii inafanya mabenki kuwa na wakati mgumu katika kuhudumia wateja wake.

“Mashauri hayo yapelekwe kwa haraka ili kuruhusu fedha hiyo kuingia kwenye mzunguko wa kibiashara,”alisema Mwaikasu

Kikao kazi hiki chenye lengo la kubaini changamoto za kibenki na mabaraza ya ardhi kinalenga kutoa suluhisho la changamoto ambazo zimejitokeza na kuathiri kwa kiwango kikubwa sekta ya benki hapa nchini. Kinajumuisha wanasheria kutoka kwenye mabenki na wenyeviti wa mabaraza ya ardhi nchini ambao jumla yao ni wajumbe zaidi ya 85.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi