Kongani ya viwanda ya SINO-TAN ni eneo la mradi wa kimkakati lililoko Kwala, Mkoa wa Pwani lenye ukubwa wa ekari 2,500. Eneo hili lina mtaji wa mwekezaji wa dola za Marekani milioni 327 (sawa na shilingi Bilioni 882), ambalo linatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 100,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 500,000.
Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema hayo leo Machi 16, 2025 katika Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari uliojikita kueleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
“Mradi huu utakapokamilika, utakuwa na viwanda vikubwa na vya kati 200 na viwanda vidogo 300 vinavyohusiana na usindikaji wa vyakula, utengenezaji wa vifaa, viwanda vya dawa, vifaa vya ujenzi, usindikaji wa viatu na nguo na pamoja na viwanda vya kemikali.” Amefafanua Msigwa.
Amesema eneo hilo litajengwa kwa awamu tano, ambapo ujenzi wa awamu ya kwanza ulianza Mei, 2022 na upo katika hatua za mwisho. Mpaka sasa kuna viwanda 3 ambavyo tayari vinazalisha na vingine 3 vipo katika hatua za mwisho za kufunga mitambo huku viwanda vingine 4 vikitarajiwa kuanza ufungaji wa mitambo ifikapo mwisho wa mwezi Aprili 2025.
“Eneo hili litakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 6 (sawa na shilingi Trilioni 16.2) kwa mwaka. Serikali itakusanya kodi na ushuru kila mwaka kwa makadirio ya shilingi trilioni 1.2,” amefafanua Msigwa.
Aidha, tangu kuanza kwa utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo, shughuli mbalimbali zimefanyika zikiwemo za ujenzi wa miundombinu ya awamu ya kwanza ndani ya eneo la mradi ambayo imekamilika kwa asilimia 80.
Msigwa ametaja shughuli ziliotekelezwa katika awamu ya kwanza kuwa ni mtandao wa barabara za zege zinazoweza kubeba malori ya mizigo, jengo litakalohifadhi kituo cha kupambana na moto pamoja na jengo la utawala litakalokuwa na ofisi za mashirika ya serikali na watoa huduma za kitaalamu. Shughuli nyingine zilizotekelezwa katika awamu ya kwanza ni mfumo wa maji ya mvua, mtandao wa umeme, mtandao wa maji safi, hifadhi za viwanda za mita za mraba 26,000, lango kuu pamoja na malazi ya wafanyakazi.
“Ili kuwezesha kuanza kwa uzalishaji wa viwanda katika eneo hilo, Serikali imefanya uunganishaji wa awali wa maji kupitia mamlaka zinazohusika kwa ajili ya matumizi ya ujenzi. Pia Serikali inaendela na mpango wa kuiunganisha kongani hii na maji ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji viwandani,” amefafanua Msigwa.
Ametaja shughuli nyingine zilizotekelezwa na Serikali kuwa ni ujenzi wa barabara za zege zinazounganisha kongani hiyo na Barabara ya Morogoro, kuunganisha mtandao wa nyaya za Fiber Optic (Mkongo wa Taifa) pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kumalizia kazi ya kuunganisha kongani hii na umeme wa Megawati 50.