Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kiwanda cha Kuunga Trekta Mkombozi wa Wakulima Wadogo
Feb 08, 2019
Na Msemaji Mkuu

                                                                                  Na: Lilian Lundo - MAELEZO

Kiwanda cha Kuunganisha Trekta aina ya URSUS kilichopo mkoani Pwani kimekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wadogo kutokana na masharti yake nafuu ya ukopeshaji wa trekta hizo.

Kutokana na masharti hayo nafuu idadi ya wakulima wadogo waodogo wanaomiliki trekta hizo kwa matumizi mbalimbali ya shughuli za kilimo imeongezeka maradufu.

Mkulima wa zao la mahindi na alizeti kutoka wilaya ya Gairo, mkoa wa Morogoro, Haji Salum ambaye alikutwa kiwandani hapo akichukua trekta aliyoinunua kwa mkopo, ameeleza kuwa ana furaha kubwa ya kumiliki chombo hicho ambacho atakitumia kulima mashamba yake pamoja na wakulima wenzake.

[caption id="attachment_40272" align="aligncenter" width="1000"] Kazi ya uunganishaji matrekta katika Kiwanda cha Kuunganisha Trekta kilichopo Kibaha mkoani Pwani ikiendelea ikiwa ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kufufua na kukuza sekta ya Kilimo hapa nchini ambapo matrekta zaidi ya 200 yameunganishwa na kuuzwa kwa wakulima mbalimbali nchini.[/caption]

"Ninayo furaha kubwa kupata chombo hiki ambacho sikutarajia kukimiliki katika maisha yangu. Ninamshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kauli mbiu yake ya ujenzi wa viwanda ambayo imetuwezesha hata sisi masikini kumiliki trekta," amesema Salum.

Mkulima huyo anayemiliki hekari 120 za mashamba ya mahindi na alizeti amesema, kwa kulima mashamba yake peke yake ana uwezo wa kurejesha fedha ambazo zimebaki kukamilisha malipo ya trekta hiyo anayoimiliki.

[caption id="attachment_40278" align="aligncenter" width="1000"] Mkulima kutoka Wilaya ya Gairo, Haji Salum akifanyia majaribio ya kuendesha trekta aina ya URSUS mara baada yakukabidhiwa trekta hilo alilonunua kutoka Kiwanda cha kuunganisha matrekta kilichopo Kibaha mkoani Pwani.[/caption]

Mkulima huyo amewashauri Watanzania kujitokeza kwa wingi kununua trekta hizo kwani masharti yake ni nafuu na zipo kwa ajili ya kila Mtanzania hata wale wenye kipato cha chini.

Aidha, mmiliki mwingine wa trekta hizo kutoka Wilaya ya Malinyi, Mkoa wa Morogoro, Jacob Mbifile ameishukuru Serikali kwa kupata trekta kwa gharama nafuu ambayo anaitumia kulima mashamba yake pamoja na wakulima wenzake kwa kuchangia kiasi kidogo kwa ajili ya marejesho ya mkopo na uendeshaji wa chombo hicho.

"Kwa sasa tunalima kwa wakati kutokana na uwepo wa trekta nyingi, tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo wakulima wengi walikuwa wakipata huduma ya kulimiwa kwa kuchelewa kutokana na uchache wa trekta zilizokuwepo hivyo kusababisha kuvuna mazao machache kutokana na kuchelewa kupanda," ameeleza Mbifile.

[caption id="attachment_40277" align="aligncenter" width="1000"] Trekta aina ya URSUS ikiendelea na kazi yakulima mashamba ya wakulima katika Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro.[/caption]

(Picha na MAELEZO)

Kwa upande wake, mkulima wa zao la punga wilayani humo Ladislaus Kidunda amesema kabla ya uwepo wa trekta hizo kulikuwa na uhaba mkubwa wa trekta hivyo kusababisha foleni kubwa ya kusubiri trekta ili kulimiwa.

"Kipindi cha nyuma tulikuwa tukipata huduma ya kulimiwa kwa trekta kwa tabu sana kutokana na wamiliki wa trekta hizo kuwapa kipaumbele wale wenye mashamba makubwa kuanzia heka 10 na kuendelea. Tofauti na ilivyo sasa ambapo wamiliki wamekuwa wengi hata sisi wenye heka mbili au tatu tunaweza kupata huduma hiyo kwa wakati," amesema Kidunda.

Nae Msimamizi Mkuu wa Kiwanda hicho, Godwin Mubi amesema mpaka tarehe 15 Januari mwaka huu, jumla ya trekta 261 zimenunuliwa kwa njia ya mkopo katika mikoa ya Manyara, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Singida na Morogoro na mikoa mingine ikiwa kwenye mchakato wa kununua trekta hizo.

"Tunakopesha trekta hizi kwa kila Mtanzania anayehitaji, ambapo hutakiwa kutoa asilimia 25 ya gharama ya trekta na gharama inayobaki atairudisha kwa kipindi cha miaka miwili. Njia nyingine ni ile ambayo mkulima anaonesha dhamira ya kupata trekta, hivyo hulipia milioni 3 hadi 4 na kiasi kinachobaki hurejesha katika kipindi cha miaka miwili," amesema Mubi.

Aidha, Mubi ameeleza vipuri vya trekta hizo za URSUS  zinapatikana kwa wingi nchini hivyo Watanzania watembelee kiwandani hapo kujua namna ya kumiliki trekta hizo kwani masharti na gharama yake ni nafuu sana.

Kiwanda cha Kuunganisha Trekta za URSUS ni kiwanda kinachosimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambapo huunganisha Trekta kutoka nchini Poland. Kiwanda hicho kilianza rasmi kufanya kazi mwezi Aprili mwaka  2017.  Uwepo wa kiwanda hicho ni matunda ya kauli mbiu ya Ujenzi wa Viwanda chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi