Na Shamimu Nyaki-WHUSM.
Serikali imesema Lugha ya Kiswahili ndio lugha ambayo inatambulisha Watanzania hivyo ni wajibu kwa Wananchi kutumia Lugha hiyo kwa usahihi katika shughuli zao za ndani na nje ya Taifa ili kukikuza na kukiendeleza .
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe alipokua akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Luninga ya Taifa ambapo ameliagiza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuandaa na kuwasilisha kwake orodha ya wahitimu wa lugha hiyo ili Serikali iwatambue.
“Lugha ya Kiswahili ni lugha ya 10 kati ya 6000 hapa Duniani, ni lazima Watanzania waone umuhimu wa kutumia lugha hii kwakua inatoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira kwa nchi ambazo zinahitaji wataalamu wa lugha hiyo,” alisema Mhe. Mwakyembe.
Aidha Dkt Mwakyembe ameeleza kuwa Sheria ya Habari imeanza kutekelezwa na vyombo vingi vya habari na wanatasnia kwa ujumla wameeilewa Sheria hiyo inayoeleza kuwa uhuru wa kutoa na kupokea habari una mipaka na ni vyema wananchi wakaelewa kuwa mitandao ya kijamii sio vyombo vya habari bali ni vyombo vya kutoa taarifa.
Hata hivyo Mhe Waziri amesema vyombo vya habari havikatazwi kuikosoa Serikali lakini vinatakiwa kukosoa kwa hoja na si kuandika habari za uongo ambazo hazizingatii weledi na taaluma ya habari.
Akizungumzia usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha usikivu wa matangazo ya Shirika hilo yanawafikia wananchi wengi zaidi,na kwa upande wa Luninga tayari inapatikana katika visimbuzi vyote.
Mhe Waziri ameongeza kuwa Mkataba kati ya Shirika hilo la Utangazaji la Taifa na Kampuni ya StarTimes umeanza kuangaliwa upya na taarifa itakapokamilika itawasilishwa kwa ajili ya hatua zinazofuata.
“Kuna kamati imeundwa kuchunguza Mkataba kati ya TBC na StarTimes na hivi karibuni viongozi wa StarTimes watakuja hapa nchini kwa ajili ya majadaliano”.Aliongeza Mhe. Mwakyembe.
Dkt.Mwakyembe ameeleza kuwa Sekta zake zote zinaendelea kufanya vizuri na sehemu ambazo zina changamoto zimeanza kutafutiwa ufumbuzi kwa kiasi kikubwa ili kufikia azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo 2025.